MUDA WA UPIGAJI KURA KATIKA UCHAGUZI WA RAIS WA IRAN WAONGEZWA

Tume ya Uchaguzi nchini Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, imeongeza muda wa kupiga kura katika uchaguzi wa duru ya 12 ya urais.
Taarifa iliyotolewa na Tume cha Uchaguzi jioni ya leo imesema kuwa muda wa kupiga kura umeongezwa hadi saa 4:00 za usiku kwa upande wa Tehran na kwa upande wa vijijini ukiongezwa hadi saa 3:00 za usiku. Imeongeza kuwa, imeamua kuongeza muda huo kutokana na mapendekezo yaliyowasilishwa kutoka vituo vya kupigia kura juu ya kuongezwa muda na baada ya Wizara ya Mambo ya Ndani kutaka kuongezwa muda wa saa mbili wa shughuli hiyo.
Upigaji kura ukiendelea kwa hamasa
Tume ya Uchaguzi ya Iran pia imeongeza muda wa saa moja wa upigaji kura wa uchaguzi wa duru ya tano ya mabaraza ya miji na vijiji. Ushiriki mkubwa wa hamasa wa wananchi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, unatajwa kuwa sababu ya kuongezwa muda huo.  Hadi tunaingia studioni, shughuli ya upigaji kura bado ilikuwa inaendelea, ambapo vituo vya kupigia kura vimeonekana kufurika kwa wingi wananchi muda wote.
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika uchaguzi wa leo
Wakati huo huo, katibu mkuu wa Umoja wa Waashuri Duniani, amesema kuwa ushiriki mkubwa wa wananchi wa Iran kutoka watu wa kila kaumu, matabaka na dini mbalimbali katika uchaguzi wa rais wa leo, ni suala lililowashangaza wengi. Yonatan Bet Kolya, ameyasema leo katika mazungumzo na Shirika la Habari la IRNA na kuongeza kuwa, umoja ulioonyeshwa na taifa la Iran katika ushiriki mkubwa wa watu kwenye upigaji kura ni suala lililowashangaza wengi duniani.

0 comments: