EU YAKATAA OMBI LA MUSEVENI NA MAGUFULI LA KUIONDOLEA VIKWAZO BURUNDI



Balozi wa Umoja wa Ulaya nchini Tanzania amekataa ombi la marais wa Tanzania na Uganda la kuutaka umoja huo uifutie vikwazo Burundi.

Roeland van de Geer amenukuliwa na mtandao wa habari wa Africa Times akitoa msimamo huo wa Umoja wa Ulaya baada ya marais wa Tanzania na Uganda kutaka kuondolewa vikwazo Burundi na kusema kuwa vikwazo hivyo vitaendelea hadi hali ya kisiasa itakapobadilika nchini humo.

Ikumbukwe kuwa katika mkutano wa kukabidhiana uenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki EAC uliofanyika jijini Dar es Salaam Tanzania siku ya Jumamosi, Rais Yoweri Museveni wa Uganda na mwenzake wa Tanzania, John Pombe Magufuli waliutaka Umoja wa Ulaya ufute vikwazo ulivyoiwekea Burundi.


Roeland van de Geer, balozi wa Umoja wa Ulaya nchini Tanzania

Mwenyekiti mpya wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Rais Yoweri Museveni wa Uganda alisema kuwa, jumuiya hiyo inapinga uamuzi wa Umoja wa Ulaya wa kumuwekea vikwazo mwanachama wa jumuiya hiyo.

Mgogoro mkubwa wa kisiasa umeikumbwa Burundi tangu Rais Pierre Nkurunziza wa nchi hiyo alipoamua kugombea tena urais kwa mara ya tatu mfululizo huku wapinzani wakisema kuwa huo ulikuwa ni ukiukaji wa wazi wa makubaliano ya Arusha, Tanzania, yaliyomaliza vita vya ndani nchini Burundi.

Uchaguzi mkuu wa Burundi ulisusiwa na wapinzani, na Umoja wa Ulaya nao ukaiwekea vikwazo nchi hiyo. Mgogoro huo umesababisha matatizo mengi yakiwemo mauaji na wimbi kubwa la wakimbizi wa ndani na nje ya Burundi.


Rais Pierre Nkurunziza wa Burundi

0 comments: