19 WAUAWA KATIKA HUJUMA YA KIGAIDI MANCHESTER, UINGEREZA



Watu wasiopungua 19 wameuawa katika mji wa Manchester nchini Uingereza kufuatia mlipuko mkubwa unaoshukiwa kuwa hujuma ya kigaidi.

Watu wengine zaidi ya 50 wanaripotiwa kujeruhiwa katika tukio hilo la Jumatatu usiku katika ukumbi wa Manchester Arena ambapo vijana wengi walikuwa wamekusanyika kutumbuizwa na muimbaji kutoka Marekani.

Walioshuhudia tukio hilo wanasema walisikia sauti ya mlipuko mkubwa baada ya muimbaji Ariana Grande, raia wa Marekani, kumaliza muziki wake.

Mkuu wa Polisi Manchester Ian Hopkins amethibitisha kuuawa watu hao 19 huku akithibtisha kuwa tukio hilo kwa sasa linatazamwa kama hujuma ya kigaidi.

Baadhi ya duru za usalama zinadokeza kuwa hujuma hiyo imetekelezwa na mlipuaji aliyekuwa amejifunga mabomu mwilini.

Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May ametoa taarifa na kusema uchunguzi unafanyika kubaini iwapo hujuma hiyo ilikuwa ya kigaidi.


Hali baada ya mlipuko Manchester

Alhamisi iliyopita Mkuu wa Idara ya Kupambana an Ugaidi katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa Jean-Paul Laborde alikuwa ameonya kuwa kuna wimbi la magaidi wa ISIS wanaorejea Ulaya baada ya kushindwa katika vita huko Iraq na Syria.

Aidha mapema mwezi huu mashirika ya kijasusi ya Uingereza yalionya kuwa raia 350 wa nchi hiyo ambao ni magaidi wanachama wa kundi la kigaidi la ISIS wamerejea nchini humo kutoka Syria na sasa ni tishio kubwa kwa usalama.

Maafisa wa usalama wanasema magaidi hao sugu ambao waliondoka Uingereza na kujiunga na kundi hilo la wakufurishaji wamekuwa wakitarajiwa kurejea nyumbani kwani ISIS imekuwa ikipata pigo Syria na Iraq na hivyo kupoteza ardhi ambazo ilikuwa imezikalia kwa mabavu.

Mashirika ya usalama  Uingereza yanasema ni vigumu kufuatilia kila gaidi aliyerejea kwani idadi yao ni kubwa na wanarejea kwa mpigo.

Hujuma ya Manchester imejiri pamoja na kuwa usalama umeimarisha Uingereza baada ya kujiri shambulizi nje ya jengo la bunge mjini London hivi karibuni ambapo watu wanne walipoteza maisha  wakati gaidi  mmoja aliendesha gari kiholela na kuwagonga wapita njia huku akimdunga kisu polisi.

0 comments: