MAKAMU WA RAIS SAMIA, AJIONEA UTIRIRISHAJI HAFIFU WA MAJI KWENYE MTO WA RUAHA MKUU

 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan ameuahidi uongozi wa Hifadhi ya Taifa ya Ruaha na wa Mkoa wa Iringa kuwa Serikali italifanyia kazi tatizo la ubovu wa barabara kutoka Iringa mjini Hadi katika hifadhi hiyo ili kuongeza idadi ya watalii katika Hifadhi ya Taifa ya Ruaha.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan ametoa kauli hiyo katika mkutano wake na Viongozi wa Hifadhi hiyo na wa mkoa wa Iringa baada ya kufanya ziara fupi katika hifadhi hiyo pamoja na kujionea utiririshaji hafifu wa maji katika Mto Ruaha uliosababishwa na shughuli za kibinadamu hasa kilimo.

Makamu wa Rais amesema serikali itahakikisha barabara hiyo inajengwa kwa awamu kwa kiwango cha lami kama hatua ya kuongeza maradufu idadi ya watalii katika Hifadhi ya Taifa ya Ruaha ambapo kutokana na ubovu wa barabara kuelekea hifadhi hapo idadi ya watalii wanaotembelea hifadhi hiyo imeendelea kupungua kila uchao.

Kuhusu vitendo vya ujangili hifadhi hapo, Makamu wa Rais ameuagiza uongozi wa hifadhi hiyo kushirikiana na wananchi wanaozunguka hifadhi hiyo ili kuwabaini majangili na kuwachukulia hatua ili kukomesha vitendo hivyo.

Amesema idadi kubwa ya majangili wanatoka miongoni mwa jamii zinazozunguka Hifadhi ya Taifa ya Ruaha hivyo wananchi wakishirikishwa kikamilifu katika kutoka taarifa za siri majangili wengi watakamatwa na kuwajibishwa.

Awali akitoa taarifa kwa Makamu wa Rais, Kuhusu utendaji kazi wa Hifadhi hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) ALLAN KIJAZI aliiomba serikali isaidie kulinusuru bonde la Usangu ili liweze kurejesha mtitiriko wa maji kwa ajili ya matumizi ya hifadhi hiyo na kumaliza mgogoro wa mpaka kati ya hifadhi na wananchi ambao umedumu kwa muda mrefu bila suluhu kupatikana.

 Amesema mapaka sasa TANAPA imeshatumia zaidi ya shilingi bilioni SABA kwa ajili ya kulipa fidia wananchi na gharama nyingine ili kunusuru bonde hilo lakini bado kuna changamoto ambazo zinaathiri usimamizi wa eneo hilo na zinahitaji maamuzi ya serikali.

Mkurugenzi huyo Mkuu wa TANAPA pia amepongeza msukumo wa dhati wa serikali ya awamu ya Tano katika kusimamia hifadhi ya mazingira na maliasili kwani jitihada hizo zitasaidia kuboresha mazingira na viumbe hai kwa ajili ya vizazi vya sasa na vijavyo.



0 comments: