ICC YATAHADHARISHA KUHUSU UKATILI UNAOFANYIKA CONGO DR

Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) imetahadharisha kuwa ukatili uliofanyika katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ikiwa ni pamoja na mauaji ya wataalamu wawili wa Umoja wa Mataifa unaweza kutambuliwa kuwa ni jinai ya kivita.
Taarifa hiyo ya mahakama ya ICC imetolewa baada ya mauaji ya karibu watu 400 wakiwemo wataalamu wawili wa Umoja wa Mataifa raia wa Marekani na Sweden katika mkoa wa katikati mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wa Kasai.  
Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai Fatou Bensouda amesema kuwa, amepokea ripoti kuhusu ukatili unaofanyika katika mapigano yamayojiri kati ya makundi ya wanamgambo na jeshi la serikali ya Congo, mauaji ya idadi kubwa ya raia, utekaji nyara na kunyongwa ovyo watu wasio na hatia. Amesisitiza kuwa vitendo hivyo vinaweza kutambuliwa kuwa ni jinai za kivita. 
Raia wengi wanaoawa Kasai, Congo
Bensouda amesisitiza kuwa hatasita kuwachukulia hatua na kuwapandisha kizimbani watu wanaohusika na uhalifu huo. 
Mkoa wa Kasai umekumbwa na ghasia tangu katikati ya mwezi Agosti, wakati askari wa kikosi cha serikali ya Congo walipomuua Kamwina Nsapu, aliyekuwa kiongozi wa wanamgambo waasi dhidi serikali kuu Rais Joseph Kabila.
Wiki iliyopita pia wanamgambo wa eneo hilo waliwaua kwa kuwakata vichwa maafisa karibu 40 wa jeshi la polisi ya nchi hiyo katika maeneo ya msituni mkoani Kasai.

0 comments: