VIONGOZI WA UMOJA WA ULAYA WAKUTANA BRUSSERS

Viongozi wa Umoja wa Ulaya wanakutana leo Machi 9, 2017 mjini Brussels katika mkutano wa kilele uliogubikwa na ajenda kadhaa ikiwemo suala la uchaguzi wa Rais wa Baraza la Ulaya.
Symbolbild EU (Getty Images/AFP/E. Dunand)
Mkutano huo wa kilele pia unatarajia kuangazia masuaala mengine ikiwa ni pamoja na suala linalohusiana na uchumi barani ulaya, hali ya sasa ya ukanda wa magharibi wa nchi za Balkan pamoja na suala la ulinzi na ushirikiano wa kijeshi.

Mkutano huo   huenda  ukawa wa mwisho viongozi wa Umoja wa Ulaya kukutana kabla ya  Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May kuanzisha rasmi mchakato wa kujitoa kwenye umoja huo kwa kutumia ibara ya 50 ya mkataba wa Lisbon.

Uingereza inatarajia kutangaza rasmi kusudio lake la kujiondoa kwenye Umoja wa Ulaya  ifikapo mwishoni mwa mwezi Machi na hivyo kuanza rasmi kipindi cha miaka miwili cha mchakato wa kujiondoa kwenye Umoja wa Ulaya.

Mkutano huo unafanyika kukiwa na mvutano kati ya Waziri Mkuu wa Poland,  Beata Szydlo  na viongozi wengine wa mataifa  yanayounda  umoja huo ambao wanaonekana kuiunga mkono hoja ya Donald Tusk kuendelea tena na wadhifa huo huku Waziri Mkuu wa Poland akimshutumu Tusk ambaye alitokea katika chama cha upinzani nchini Poland cha Civic Platform (PO)  na alikuwa afisa wa serikali nchini Poland kwa kujihusisha na siasa za ndani za Poland.

Hata hivyo kwa upande wake  Tusk amesema yuko tayari na anasubiri uamuzi wa viongozi wa mataifa 28 yanayounda Umoja wa Ulaya katika kuelekea uchaguzi huo huku pia akikanusha hoja zilizoibuliwa na waziri mkuu wa Poland,  Beata Szydlo kuwa amekiuka taratibu zake za kazi kwa kuingilia siasa za ndani za Poland.

Tusk amesisitiza kuwa hausiki hata kidogo na migongano hiyo na kuwa haiegemei upande wowote na wala hatarajii kufanya hivyo hata katika siku za usoni.

Serikali ya Poland ambayo haiuangalii kwa jicho jema Umoja wa Ulaya na ambayo imekuwa ikirumbana na Umoja wa Ulaya juu ya utawala wa sheria  Jumamosi iliyopita ilipendekeza jina la Mbunge wa Ulaya, Jacek Saryusz- Wolsk kuwania nafasi hiyo badala ya Donald Tusk.

Tusk apewa nafasi kubwa ya kuchaguliwa tena 
Großbritannien EU-Ratspräsident Donald Tusk (picture-alliance/dpa/A. Rain) Rais wa sasa wa baraza la ulaya Donald Tusk
Ujerumani  kwa upande  wake imesema kuna dalili njema  za kuchaguliwa tena kwa Tusk  ambaye kipindi chake cha sasa cha uongozi  kinamalizika mwezi Mei kuendelea kuwa Rais wa Baraza la Ulaya mnamo wakati wanadiplomasia wa ulaya wakiishutumu serikali ya Poland kwa kutaka kuhusisha  masuala ya ndani na masuala ya kimataifa.

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amesema kuchaguliwa kwa Tusk ni ishara ya uthabiti ndani ya Umoja wa Ulaya.
Mvutano huo kati ya serikali ya Poland  na Umoja wa Ulaya unaelekea kuleta mgawanyiko katika kipindi ambacho viongozi wa umoja huo wametoa mwito wa kuimarishwa umoja mnamo wakati Uingereza ikijiandaa kuanzisha rasmi mchakato wa kujiondoa kwenye umoja wa ulaya.

0 comments: