TUNA VITU VINNE MUHIMU TUMESHINDWA KUVITUMIA

Julian Msacky

WAKATI wa uhai wake, Mwalimu Julius Nyerere alitupa somo muhimu kuwa ili tuendelee tunahitaji vitu vinne. 

Uongozi bora, siasa safi, ardhi na watu. Huu ni mtaji muhimu kwa nchi yoyote inayotaka kupiga hatua kimaendeleo.

Kwa nchi yangu Tanzania Mungu ameijalia ardhi na watu. Vitu hivi viwili vipo vya kutosha, lakini vinatumika inavyotakiwa?

     Hayati Mwalimu Julius Nyerere
Ni kwa namna gani vinatumika vizuri kuharakisha maendeleo ya nchi na kukuza uchumi wa nchi na mtu mmoja mmoja.

Tuelewe vipi kwa mfano tunapoambiwa uchumi wetu umekuwa lakini neema hiyo haionekani kwa wananchi?.

Ni baba gani anakuwa tajiri (uchumi mzuri), lakini familia yake inaishi maisha ya kubangaiza asubuhi hadi jioni? 

Tunadhani uchumi unapokua unatakiwi uonekane kwa wananchi wa kawaida lakini kama si hivyo lazima yawepo maswali.

Mwananchi asiyeweza kumudu milo mitatu kwa siku utamwambia uchumi wa nchi umekua wakati lishe inamshinda.

Kwenye ardhi yetu tunaitumia ipasavyo? Tunaitumia vizuri kwa ajili ya kilimo bora kama tunavyoimba au imejikalia tu?

Kama tungetumia ardhi yetu vizuri leo hii habari za ukosefu wa chakula ingetoka wapi? Habari ya njaa ingetoka wapi?

Binafsi naamini ardhi yetu haijatumika vizuri ndiyo maana wafugaji na wakulima wanavimbiana kila kukicha.

Kwa ardhi tuliyonayo tunashindwa nini kuipangilia vizuri ili wafugaji wafuge kwa amani na utulivu ndani ya nchi yao?

Ukubwa wa ardhi uliopo ni aibu kuona wakulima na wafugaji wanashikana mashati kwa sababu hii na ile. 

Hili ni eneo ambalo hajaweza kulitumia vizuri kiasi kwamba watu wanajazana mijini kwa sababu ya ubunifu mdogo.

Kwa miaka mingi sasa tumeshindwa kuifanya ardhi yetu kuwakomboa wananchi kiuchumi kwa sababu haijapimwa.

Tatizo ni kwamba uongozi bora haupo. Tunapokosa uongozi bora maana yake mambo yetu yanafanyika ovyo ovyo.

Yanakuwa hivyo kwasababu viongozi hawajitambui. Hawajui majukumu yao kwa wananchi ni yapi. Kwa hili kuna ombwe.

Matokeo yake idara nyingine zinajiendesha kwa kulegalega na kimazoea na hivyo kujishindwa kusonga mbele.

Kwa mfano, ngazi ya halmashauri zetu hiki kinachoitwa uongozi bora upo kwa jina au tumekuwa maharibi wa kuzunguka ofisini? 

Ni ofisa gani wa halmashauri leo hii anajua mkulima analima kitu gani? Ni ofisa gani anajua mfugaji anafuga nini na kwa vipi?

Tembelea wananchi uone wanavyopata hasara kwa kukosa wa kumwelekeza alime nini kwenye eneo lake.

Ardhi iliyotakiwa kulima muhogo analima chai. Ardhi iliyotakiwa kulima viazi analima katani. Ni tatizo kweli kweli.

Nenda kwa wafugaji. Wanapoteza mifugo kwa magonjwa yanayoepukika kwa vile tu amekosa kuelekezwa tiba ni nini.

Ndiko tulikofikia kama nchi wakati tunatamani kuwa nchi ya viwanda. Kwa hali hii itawezekana kweli?

Mahali ambapo wakulima wanalima wasichoweza kuvuna na kufuga wasichoweza kupata. Hii ni shida.

Tunahitaji uongozi bora ili kutuondoa hapa tulipo. Uongozi bora haupimwi kwa matamko au lugha kali majukwaani.

Uongozi bora hupima kwa namna watendaji wanavyotimiza majukumu yao kama sheria na taratibu za kazi zilivyo.

Ikumbukwe mahali pasipo na uongozi bora (good leadership) hata ashuke malaika ni vigumu kupata maendeleo. 

Kuna umuhimu suala hili likasisitizwa kuanzia shuleni ili taifa liondokane na ukame wa viongozi bora.

Tukiwa na viongozi bora kilimo kitakwenda vizuri, wafugaji watafuga vizuri, elimu itakuwa bora na mambo mengine mengi.

Ili yote hayo yawezekane ni lazima tuwe na siasa safi. Kwa maana ya kukubali mawazo tofauti ili kusonga mbele.

Kupitia siasa tutashauriwa namna gani tuunganishe nguvu kukabiliana na changamoto zilizopo.

Ni muhimu kwa sababu haijawahi kutokea mawazo ya wateule wachache yakaleta rutuba katikati ya kundi la watu.

Ndiyo maana hata Yesu aliwashirikisha wanafunzi wake ili kutengeneza fikra pana kwa lengo la kuinjilisha vizuri.

0 comments: