TANZANIA KUPATA MEGAWATI 400 ZA UMEME KUTOKA ETHIOPIA

A 4
Na Daudi Manongi-MAELEZO.
Tanzania inategemea kupata Megawati 400 za umeme kutoka Ethiopia ikiwa ni moja ya makubaliano yaliyofikiwa baada ya ziara ya kikazi ya siku mbili ya Waziri Mkuu wa Ethiopia Mhe.Haile Mariam Desalegn. 
Hayo yamesemwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt John Pombe Magufuli alipokuwa akizungumza na vyombo vya habari juu ya makubaliano na mikataba ambayo nchi za Tanzania na Ethiopia wametiliana saini leo Ikulu Jijini Dar es Salaam.
“Tukitaka kujenga uchumi wa viwanda ni lazima tuwe na umeme wa kutosha,wenzetu Ethiopia wametuonyesha njia na mimi nimemuomba Mhe.Waziri atusaidie wataalamu kutoka nchini kwake ili  waje  tuwaonyeshe maeneo mbalimbali watusaidie katika kupata umeme wa uhakika kwa kujenga mabwawa ya umeme ambayo yamesaidia sana katika kupatikana kwa umeme wa kutosha nchini kwao.”Aliongeza Rais Magufuli.
Aidha amesema kuwa kupatikana kwa umeme huo kutasaidia kuleta changamoto kwa shirika la umeme nchini katika kuwapatia wananchi bei ya chini na hivyo kuleta ushindani katika upatikanaji wa umeme nchini.
Kwa upande wake Waziri Mkuu wa Ethiopia Mhe.Haile Mariam Desalegn amesema kuwa wana mengi ya kujifunza kutoka Tanzania kwani nchi hizi mbili zina historia inayofanana na kuongeza kuwa hakuna haja ya wao kwenda nje ya Afrika kupata uzoefu katika masuala mbalimbali.
Ameongeza kuwa lengo kuu la kuja nchini ni kwa sababu anahamini nchi hizi mbili zinaweza kuunganisha nguvu zake na kuwa nguzo kuu katika maendeleo katika eneo la ukanda wa Afrika Mashariki na kati.
“Tanzania na Ethiopia ni nchi ambazo zina ushirikiano mzuri sana,sisi sio washindani bali tunasaidiana katika masuala mbalimbali kwani tumekuwa katika hatua mbalimbali za kuwaondoa wananchi wetu katika umaskini katika hatua zinazofanana,na huu ni wakati muafaka katika kuimarisha ushirikiano wetu kwa faida ya watu wetu kwa ujumla”Alisisitiza Mhe.Desalegn.






0 comments: