SUMATRA YAWAPIGA MSASA WADAU WA ZIWA TANGANYIKA MKOANI KIGOMA

Na Magreth Magosso,Kigoma


MKURUGENZI  Mkuu wa  Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Nchi kavu na Majini (SUMATRA), Giliard Ngewe amewataka wadau wa  Vyombo vya usafirishaji wa abiria na mizigo katika Ziwa Tanganyika Mkoa wa Kigoma, wazingatie sheria, kanuni na weledi katika shughuli zao ili kupunguza  ajali zinatokea kila wakati katika ziwa hilo.
                                                       
Akithibitisha hilo jana Kigoma Ujiji, kwenye ufunguzi wa mafunzo ya siku mbili juu ya kukumbushwa wajibu wao kwa mujibu wa sheria, taratibu na kanuni za usafirishaji kwa abiria na mizigo ni pamoja na undaji wa boti zenye kiwango cha ubora wenye kiwango kwa mujibu wa sumatra  ,ili kuimarisha uchumi wa shughuli hizo katika mkoa huo.

Ngewe alisema katika kipindi cha januari mwaka 2013 hadi januari 2017 zaidi ya  watu 50 wamepoteza maisha sanjari na kupoteza mizigo hali inayochangiwa na boti duni ambazo zinashindwa kuhimili uhalisia wa mabadiliko ya tabia nchi yanayojitokeza katika ziwa hilo.

“Sumatra imejiwekea utaratibu wa kuwajengea uwezo wadau wake kwa kubadilishana taaluma miongoni mwao kwa wavuvi, wamiliki wa zana za uvuvi na mafundi maboti kila kona ya mkoa husika kwa kushirikiana na wataalamu kutoka chuo cha uvuvi cha Mbegani (FETA) kuimarisha kiwango bora cha chombo husika” alifafanua Ngewe.

Kwa upande wa Mgeni rasmi  ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya kigoma, Samsoni Anga kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa hapo, Emanueli Maganga  aliema wadau hao hawana budi kutii sheria zilizopo kwa mujibu wa Sumatra na kuwataka abiria wavae vifaa vya uokoaji (lifejacket) ili kujiokoa na ajali zisizotabirika.

Anga, alieleza kuwa watakaokiuka sheria za usafirishaji watawajibishwa katika vyombo vya sheria ,kwa kuwa vifo vikitokea huwajibika katika hilo na kuwasihi wazingatie sheria na taratibu za usafirishaji wa abiria na mizigo kwa mujibu wa uimara wa chombo chake na idadi ya uzito wa mzigo na abiria kwa ujumla.

Aidha aliwakumbusha wawatumie wataalamu wa hali ya hewa waliopo katika mkoa huo ili kufanya shughuli zao kwa uhakika na waachane na tabia ya mazoea katika usafirishaji wa abiria na mizigo sanjari na kutosafirisha abiria kinyemela hali inayochangia vifo visivyojulikana .

Kwa upande wa mmiliki wa boti za uvuvi, Maftaha Bahila alisema changamoto kubwa ni mitaji ya kuwezesha boti za kisasa na wanaogopa kuunda vikundi vya ushirika kutokana na uaminifu mdogo baina ya wadau wa vyombo husika na kuiomba serikali iwapatie mikopo isiyokuwa na riba kubwa ili kuboresha shughuli za uvuvi na usafirishaji wa mizigo na abiria.

0 comments: