SHAMBULIO LA KUNDI LA KIGAIDI KWENYE VITUO VYA MAFUTA NCHINI LIBYA

Sambamba na kuendelea migogoro ya kisiasa na kutokuwepo usalama nchini Libya, kwa mara nyingine kundi moja la wabeba silaha limeweza kudhibiti kituo cha mafuta katika eneo linalojulikana kwa jina maarufu la 'Hilali ya Mafuta' kaskazini mashariki mwa Libya.
Kundi la wabeba silaha linaloitwa 'Vikosi vya Ulinzi wa Benghazi' limedhibiti kituo hicho muhimu cha mafuta ingawa hadi sasa bado mapigano yanaendelea. Kundi hilo limesonga mbele hadi eneo lenye vifaru vya kisasa na rada ya kuzuia mashambulizi ya anga eneo la uwanja wa ndege wa Ra's Lanuf. Hii ni katika hali ambayo, miezi michache iliyopita, kwa kuungana makundi ya kijeshi ya nchi hiyo, yaliweza kuliondoa kundi la kigaidi na ukufurishaji la Daesh, kutoka maeneo liliyokuwa linayadhibiti. Hata hivyo kuendelea tofauti baina ya makundi ya kisiasa nchini humo, kumetoa mwanya mpya kwa kundi la kigaidi la 'Vikosi vya Ulinzi wa Benghazi' kuchukua nafasi ya kundi la Daesh na kudhibiti kituo hicho cha mafuta.
Askari wa serikali ya Libya
Wakati huo huo serikali ya umoja wa kitaifa yenye makao yake mjini Tripol, magharibi mwa Libya, imetangaza kutohusika na mizozo ya kijeshi katika eneo la Hilali ya Mafuta. Hii ni katika hali ambayo kikosi cha ulinzi wa vituo vya mafuta nchini Libya kilicho chini ya kamanda Khalifa Haftar, ambaye ni mkuu wa jeshi la nchi hiyo na aliye chini ya serikali yenye makao yake mashariki mwa nchi hiyo, hakiikubali serikali ya umoja wa kitaifa yenye makao yake mjini Tripoli. Inafaa kukumbusha kuwa, tarehe 12 Septemba mwaka jana, Haftar aliongoza operesheni kali za kijeshi katika eneo la Hilali ya Mafuta na kufanikiwa kudhibiti vituo vya mafuta vya Al-Zuwaitina, al-Bariqah, Ra's Lanuf na al-Sidr. Hivi sasa genge la kigaidi la Vikosi vya Ulinzi wa Benghazi lenye mafungamano na mtadao wa kigaidi wa al-Qaidah, linakusudia kuliteka eneo hilo ili lipate fedha za kugharamia operesheni zake za kigaidi nchini Afghanistan, Misri na hata katika nchi za Ulaya. Libya ilitumbukia katika mgogoro wa ndani hapo mwaka 2011 baada ya kuondolewa madarakani serikali ya Kanali Muammar Gaddafi, kufuatia uingiliaji wa baadhi ya madola ya Kiarabu na Muungano wa Kijeshi wa Nchi za Magharibi (NATO). Uingiliaji huo ndio uliotoa mwanya wa kuendelea machafuko ya ndani sambamba na kujipenyeza katika nchi hiyo yenye utajiri wa mafuta, makundi ya kigaidi likiwemo la Daesh. Libya inakabiliwa na hatari kubwa hivi sasa hata kwa kuongezeka machafuko ya muda mrefu sasa, na pia kuweko makundi ya wanamgambo ya kigaidi hususan katika maeneo yenye migogoro. Isisahaulike kuwa, Libya ni moja ya nchi muhimu na mzalishaji mkubwa wa mafuta katika soko la dunia. Bajeti yake inadhaminiwa kupitia nishati hiyo muhimu. 
Askari wa Libya wakielekea kupambana na magaidi
Isisahaulike kuwa, iwapo maeneo hayo ya yenye utajiri wa mafuta yatatekwa na magenge ya kigaidi, kutazorotesha mno uchumi dhaifu wa nchi hiyo baada ya jambo hilo kuikatia Libya vyanzo vyake vya kifedha. Mbali na tishio la makundi ya kigaidi, hivi sasa Libya inakabiliwa na hatari nyingine ya kugawika vipande vipande. Si hayo tu, lakini pia mizozo ya kisiasa baina ya makundi tofauti bado inaendelea. Hadi hivi sasa na licha ya upatanishi wa nchi tofauti za kieneo wa kuwakutanisha viongozi tofauti wa Libya, lakini bado hakujafikiwa makubaliano chanya. Ni hivi karibuni tu ambapo bunge na serikali yenye makao yake huko mashariki mwa Libya, lilikataa pendekezo la Misri la kutaka kuwa mpatanishi. Vita na mapigano ya ndani ya kuwania madaraka nchini humo si tu kwamba vimetoa nafasi ya kujistawisha makundi ya kigaidi, bali pia kumetoa mwanya wa uingiliaji wa masuala ya ndani kwa nchi za Magharibi na baadhi ya nchi za eneo hilo.
Nchi hizo zinafanya njama sambamba na kutoa uungaji mkono wa siri kwa makundi ya kigaidi, kuendeleza moto wa vita na tofauti nchini Libya na hata katika eneo zima la kaskazini mwa Afrika, ili kwa njia hiyo ziweze kupanua ushawishi wao katika eneo hilo. Ni kwa ajili hiyo, hujuma iliyoendana na udhibiti wa kituo cha mafuta cha eneo la Hilal ya Mafuta, kumeyafanya makundi ya kisiasa kutahadharisha juu ya njama za kuharibu juhudi kwa ajili ya kufikiwa makubaliano ya usalama na amani nchini humo.

0 comments: