Mwakilishi wa Ujerumani anayesimamia kamati ya Ulaya inayoshughulikia uhusiano na nchi za nje Josef Janning amesema siasa za Marekani hazijawahi kuwa za kutatanisha kama ilivyo sasa. Kwa upande wake Profesa John Harper wa chuo kikuu cha Johns Hopkins cha Bolgna na mtaalamu wa sera za nje za Marekani amesema kansela Merkel atapaswa kutafuta njia mpya ya kujaribu kuanzisha uhusiano wa kikazi na rais Trump. Profesa huyo amesema rais Trump anatofautiana sana na marais wa Marekani wa hapo awali Barack Obama na George Bush kwa sababu Trump hakuwa na uzoefu wa kuendesha serikali kabla ya kuwa rais.
Bwana Josef Janning amesema lengo la Kansela Merkel ni kupata angalau kauli thabiti ya rais Trump juu ya mchakato wa nchi zilizoendelea kiviwanda na zile zinazoinukia kiuchumi G-20 na juu ya haja ya kuyashughulikia maswala kwa njia ya ushirikiano. Naye Profesa Harper anasema anatumai kuwa Kansela Merkel atafanikiwa kumshawishi rais Trump aache kuushutumu Umoja wa Ulaya na pia aache kuwaendekeza wanasiasa kama Marine le Pen wa Ufaransa. Ni vigumu kubainika katika mkutano wa kwanza wa viongozi wa Ujerumani na Marekani iwapo watakubaliana msingi wa kufanya kazi kwa pamoja. Hata hivyo kansela wa Ujerumani aliliambia gazeti moja la hapa nchini Ujerumani "Saarbruecker" kwamba wakati wote ni vizuri kujadiliana badala ya kumjadili mtu. Bibi Merkel amesema Ujerumani na Marekani zitanufaika ikiwa zitashirikiana vizuri na kwa haki.
0 comments: