KAMATI YA BUNGE YAIPONGEZA HOSPITALI YA TAIFA MUHIMBILI KWA KUBORESHA HUDUMA ZA AFYA
Posted by khamisimussa77@gmail.com at 9:58 PM
Mkurugenzi
Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Profesa Lawrence Museru
akitoa taarifa fupi ya utendaji kwa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya
Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii.ambayo imeitembelea hospitali hiyo jana. Kutoka kushoto ni Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii,
Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Hamisi Kingwangallah na Mwenyekiti wa kamati
hiyo Peter Serukamba.
Baadhi ya Wajumbe wa kamati hiyo wakifuatilia ripoti ya utendaji iliyotolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa MNH, Profesa Museru.
Naibu
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Hamisi
Kingwangalla (kushoto), Mwenyekiti wa kamati hiyo, Peter Serukamba na
Mkurugemzi Mtendaji wa MNH, Profesa Museru wakisiliza maoni ya wajumbe
wa kamati hiyo jana.
Mjumbe
wa Kamati hiyo, Dk Faustin Ndugulile akitoa maoni yake baada ya
mkurugenzi wa hospitali hiyo kuwasilisha taarifa ya utendaji ya
hospitali hiyo kwa wajumbe.
Baadhi
ya wakurugenzi, wakuu wa idara wa hospitali hiyo wakifuatilia taarifa
ya utendaji ya MNH iliyotolewa jana kwa wajumbe wa kamati hiyo.
Wajumbe wa kamati hiyo wakikagua jengo ambalo litatumika kutoa tiba kwa wagonjwa wa figo.
Mkuu
wa Idara ya Magonjwa ya Dharura na Ajali katika Hospitali ya Taifa
Muhimbili (MNH), Dk Juma Mfinanga akiieleza Kamati ya Kudumu ya Bunge ya
Huduma na Maendeleo ya Jamii jinsi huduma ya telemedicine inavyofanya
kazi baada ya kuunganishwa na hospitali nyingine za mikoa. Kushoto ni
Mwenyekiti wa kamati hiyo Peter Serukamba, Mjumbe Joseph Mbilinyi
(katikati), Mjumbe Mussa Hassan Zungu na Zitto Kabwe.
………………
Na John Stephen, MNH
Kamati
ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii imeipongeza
Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) kutokana na ubunifu wa kufanya
mageuzi makubwa ya kuboresha huduma za afya.
Kauli
hiyo imetolewa jana na Mbunge wa Viti maalumu Mkoa wa Njombe, Mheshimiwa
Lucia Mlowe wakati akichangia taarifa ya utendaji iliyowasilishwa kwa
kamati hiyo na Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali hiyo, Profesa Lawrence
Museru.
“Napenda
kuwapongeza viongozi na wafanyakazi wa MNH kutokana na ubunifu wenu
mkubwa mnaofanya katika kuleta maendeleo ambayo yamelenga kutoa huduma
bora. Kutokana na juhudi hizi Serikali inapaswa kutoa fedha ilizoziahidi
kwa MNH.
“Nchi nzima inaitegemea MNH, Serikali ione huruma kwa MNH iwapelekee fedha, isiwaache pekee yao,” amesema Mlowe.
Mjumbe
wa kamati hiyo msheshimiwa Faustin Mdugulile ameipongeza MNH kutokana
na mageuzi makubwa ya kuboresha huduma za afya na ameahidi kuisema MNH
bungeni ili serikali kushughulikia changamoto zinazoikabili hospitali
hiyo.
Naye
Mwekiti wa Kamati hiyo Peter Serukamba ameitaka MNH kuwashirikisha wadau
wa afya katika kutoa huduma za afya ili kupunguza gharama za
uendeshaji.
“Naishauri
serikali iwaachie wadau wa afya kusimamia vifaa tiba zikiwamo mashine
za CT-Scan, MRI na vikiwamo vifaa vingine ili kupunguza gharama za
uendeshaji. Nchi nyingine za ulaya wanatumia njia hii kuendesha
hospitali na lengo ni kupunguza gharama,” amesema Serukamba.
Awali
kabla ya wajumbe wa kamati hiyo kuzungumza, Mkurugenzi Mtendaji wa
hospitali hiyo Profesa Museru amesema MHN imeanza ukarabati wa majengo
ya kutolea huduma za upasuaji kwa kina mama.
Amesema
kutokana na ukarabati huo, vyumba vya upasuaji vimeongezeka kutoka
vyumba viwili hadi wanne, kwenye jengo la upasuaji vyumba vimeongezeka
kutoka saba hadi vinane na jengo la watoto vyumba viwili hadi hadi
vinne.
Profesa
Museru amesema katika mwaka wa fedha 2016/17, hospitali inaendelea na
mkakati wa kuongeza vitanda vya wagonjwa mahututi kutoka vitanda 17 hadi
kufikia vitanda 77.
Amesema
kwamba katika kipindi cha Julai hadi Desemba 2016, hospitali imetumia
Sh. 59.650 bilioni na kwamba Sh. 24.512 bilioni zilitumika kwa matumizi
ya kawaida wakati Sh.29.888 bilioni 29.888 zilitumika kulipa mishahara
ya wafanyakazi.
“Sh.
5.250 bilioni zilitumika kwa ajili ya miradi ya maendeleo ikilinganishwa
na sh. 51.017 bilioni ambazo zilizotumika katika kipindi cha Julai
mpaka Disemba 2015 ambapo sh. 19.222 bilioni zilitumika katika matumizi
ya kawaida, sh. 30.703 bilioni zilitumika kulipa mishahara ya
wafanyakazi na sh. 1.092 bilioni zilitumika katika shughuli za miradi ya
maendeleo,” amesema Profesa Museru.
Picha na John Stephen, Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments: