ZARIF: KUINGIA WANAJESHI WA MAREKANI NCHINI SYRIA KUTAZIDISHA MGOGORO

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema, mpango wa serikali ya Marekani wa kutuma wanajeshi wake nchini Syria hautakuwa na matokeo mengine ghairi ya kuongeza mgogoro katika eneo la Mashariki ya Kati na duniani kiujumla. Amesema hayo pambizoni mwa mkutano wa usalama uliofanyika mjini Munich, Ujerumani wakati alipohojiwa na televisheni ya CNN.
Kwa mujibu wa shirika la habari la IRNA, Muhammad Javad Zarif amekumbushia hatua ya Marekani ya kuishambulia na kuikalia kwa mabavu Iraq na kusema kuwa, uvamizi huo wa Marekani nchini Iraq ndio uliozaa genge la kigaidi la Daesh (ISIS).
Amesema, kuweko wanajeshi wa kigeni nchini Syria kutayatia nguvu magenge ya kigaidi ambayo yatatumia fursa hiyo kushawishi vijana wengi zaidi kujiunga nayo. Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameongeza kuwa, wale ambao wameanzisha genge la kigaidi la Daesh ndio hao hao waliokuwa wamempa silaha dikteta wa Iraq Saddam Hussein na ndio wao walioanzisha mtandao wa al Qaida.
Muhammad Javad Zarif, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran

Kwa upande wa hatua za kiadui za Marekani dhidi ya Iran, Zarif amesema, mtu yeyote ayaneijua historia ya Iran anaelewa vyema kwamba Wairani kamwe hawababaishwi na kauli za vitisho na njia pekee ya kupata majibu mazuri kutoka kwa Wairani ni kuheshimiana na kulinda manufaa ya pamoja.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran aidha amesema, serikali ya Barack Obama huko Marekani iliamua kutumia vikwazo vya kiuchumi kudhihirisha chuki za Marekani dhidi ya taifa la Iran lakini mwenyewe alilazimika kufanya mazungumzo na Iran kuhusu miradi yake ya nyuklia baada ya kufeli vikwazo vyake hivyo.
Amesema, jamii ya kimataifa inakubaliana kwa kauli moja kuhusu umuhimu wa makubaliano ya nyuklia yaliyofikiwa baina ya Iran na kundi la 5+1 na kuongeza kuwa, watu wote wakiwemo wataalamu wa Marekani wanatambua vyema kuwa JCPOA ni makubaliano bora zaidi ya nyuklia na hayana faida kwa Iran pekee, bali hata kwa Marekani.

0 comments: