WAZIRI MKUU AONYA WATAKAOPOKEA RUSHWA KWA WAFANYABIASHARA DAWA ZA KULEVYA

 
Na Beatrice Lyimo-MAELEZO
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa amesema kuwa hatua kali zitachukuliwa kwa atakayepokea rushwa kutoka kwa wauzaji, wasambazaji na watumiaji wa Madawa ya Kulevya.

Ameyasema hayo leo jijini Dar es salaam wakati wa uzinduzi wa kikao cha kwanza cha Baraza la Taifa la kudhibiti dawa za kulevya nchini.

“Sheria ya udhibiti wa madawa ya kulevya itumike vizuri, Serikali na Baraza halitahitaji mtu yeyote mwenye mamlaka kupokea rushwa ikigundulika hatua kali zitachukuliwa” alifafanua Waziri Mkuu Majaliwa.

Waziri Mkuu alisisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kuendelea kuimarisha mapambano dhidi ya udhibiti wa Dawa za Kulevya nchini ambayo yamekuwa yakifanywa na Serikali za Awamu zilizotangulia.

Aidha, Waziri Mkuu alisema kuwa mapambano dhidi ya Dawa za Kulevya ni vita inayotakiwa kupigana kwa nguvu kubwa kwani madhara ya dawa hizo ni kubwa kwa jamii hususani vijana ambao ni nguvu kazi ya taifa.

“Tunahitaji ushirikiano wa karibu wa pande zote mbili za Muungano kwani tatizo hili limeathiri pande zote na ukanda wa bahari unatumika sana kama njia ya kuingiza dawa hizo” 

“Wakuu wa Mikoa mna kazi kubwa katika vita hii, mkiwa wenyeviti wa Kamati za Ulinzi na Usalama mpo kwenye nafasi nzuri ya kuendesha vita hii kwa mujibu wa Sheria, Kanuni na Taratibu zilizopo” alisema Waziri Mkuu.

Hata hivyo Waziri Mkuu alibainisha kuwa, wajibu wa Baraza ni kusimamia utekelezaji wa Sera ya Udhibiti wa Dawa za Kulevya nchini, ambapo jukumu hilo ni kubwa na wajumbe wa Baraza hilo wanatakiwa kulitekeleza kwa uadilifu na umahiri mkubwa.

Baraza la Taifa la kudhibiti Dawa za Kulevya limeanzishwa chini ya kifungu cha 5 cha Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Na. 5 ya mwaka 2015 ambapo Waziri Mkuu ndiye Mwenyekiti wa Baraza hilo pamoja na wajumbe wengine wakiwemo Waziri anayeshughulikia Mambo ya Sheria, Waziri anayeshughulikia Mambo ya Ndani ya Nchi.

Wengine ni Waziri anayeshughulikia Afya, waziri anayeshughulikia Maendeleo ya Jamii, Waziri anayeshughulikia Mambo ya Nchi za Nje, Waziri anayeshughulikia Fedha, Waziri anayeshughulikia Maendeleo ya Vijana, Waziri anayeshughulikia Elimu, Waziri anayeshughulikia Kilimo, Waziri anayeshughulikia Uchukuzi na Waziri anayeshughulikia Ulinzi.

0 comments: