WASWAHILI WA BURUNDI WALALAMIKIA KUTENGWA KATIKA MAZUNGUMZO YA AMANI YA ARUSHA

Wakati mazungumzo ya kusaka amani nchini Burundi yanaendelea mjini Arusha, kaskazini mwa Tanzania, makundi mbalimbali ya kijamii kutoka Burundi yametoa wito wa kutaka kushirikishwa katika mchakato huo wa kuupatia ufumbuzi mgogoro huo wa kisiasa.
Hayo yamekuja baada ya Waswahili wanaounda jamii ndogo ya raia wa Burundi kufanya maandamano mbele ya ukumbi kunakofanyika mazungumzo hayo jijini Arusha, wakitaka nao wajumuishwe kwenye meza ya mazungumzo hayo.
Sehemu ya ujumbe wa jamii ya Waswahili walioandamana
Kadhalika jamii hiyo, imemtaka rais wa zamani wa Tanzania, Benjamin Willium Mkapa, kutolipuuza suala hilo na kutishia kuwa hawatokuwa tayari kukubaliana na maamuzi ya mazungumzo ambayo yamewatenga. Hata hivyo polisi ya Tanzania imewatia mbaroni waandamanaji kadhaa kati yao. Ni vyema kuashiria kuwa, tangu kulipotiwa saini makubaliano ya amani ya mjini Arusha miaka kadhaa iliyopita na ambayo yalihitimisha vita vya miongo kadhaa nchini Burundi, jamii ya Waswahili wa nchi hiyo imekuwa ikilalamikia kile inachokisema kuwa ni kusahaulika na kutengwa katika mchakato huo.
Viongozi wapatanishi katika mgogoro wa Burundi
Kadhalika jamii hiyo inadai kuwa, kuendelea kutengwa katika maamuzi ya kuainisha mustakbali wa taifa la Burundi, ni kuzidi kupalilia mzozo ambao unaweza kuibuka wakati wowote. Katika vita vya kikabila baina ya jamii ya Watutsi na Wahutu nchini Burundi, maelfu ya watu waliuawa na wengine wengi kuwa wakimbizi nje ya nchi hiyo mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

0 comments: