WAISLAMU WA MAREKANI WASAIDIA KIFEDHA KUKARABATI MAKABURI YA MAYAHUDI YALIYOBOMOLEWA

Waislamu nchini Marekani wamechangisha maelfu ya dola kusaidia ukarabati wa makaburi ya Mayahudi yaliyobomolewa katika jimbo la Missouri.
Kampeni hiyo iliyoanzishwa siku ya Jumanne kwa anuani ya "Umoja wa Waislamu kwa ajili ya kukarabati makaburi ya Mayahudi" hadi kufikia jana iliweza kukusanya zaidi ya dola 91,000 za Kimarekani japokuwa lengo la awali lilikuwa ni kukusanya dola 20,000.
Mchango huo wa fedha umetolewa kusaidia kukarabati eneo la kihistoria la makaburi ya Mayahudi ambayo yalibomolewa katika hujuma iliyofanywa wiki iliyopita.
Taasisi ya Kiislamu iliyoanzisha mchango huo imeeleza kuwa katika kuonyesha mshikamano na jamii ya Mayahudi ya Marekani Waislamu wa nchi hiyo wanalaani kitendo hicho cha kuvunjia heshima eneo hilo la makaburi.
Mawe ya makaburi yaliyobomolewa
Taarifa hiyo imeongeza kuwa lengo kila hatua ni kudhihirisha "maisha na shakhsia ya Bwana Mtume Muhammad SAW" na kufikisha ujumbe kuwa vitendo vya aina hiyo vya uenezaji chuki na uvunjiaji heshima matukufu ya kidini havina nafasi ndani ya jamii ya Marekani.
Kwa mujibu wa Polisi ya jimbo la Missouri zaidi ya makaburi 170 yamebomolewa katika hujuma hiyo.
Hujuma hiyo imefanywa katika hali ambayo vitisho vya utegaji mabomu vimetolewa dhidi ya vituo kadhaa vya Mayahudi katika maeneo mbalimbali ya Marekani.
Ripoti zinaeleza kuwa tangu ulipoanza mwaka huu wa 2017 hadi siku ya Jumatatu iliyopita vimetolewa vitisho visivyopungua 69 vya utegaji mabomu dhidi ya vituo 54 vya Mayahudi katika nchi za Marekani na Canada. 
Tayari Polisi ya Upelelezi ya Marekani (FBI) imeanzisha uchunguzi juu ya suala hilo.../

0 comments: