TIMU YA USALAMA WA TAIFA YA MAREKANI YAKUMBWA NA MGOGORO

Kufuatia uamuzi wa Robert Harward kukataa ombi la Rais Donald Trump wa Marekani la kusimamia usalama wa taifa, timu ya usalama ya rais huyo imeingia katika hatua mpya ya mgogoro ambao haujawahi kushuhudiwa katika historia ya Ikulu ya White House.
Katika kipindi cha chini ya mwezi mmoja tokea serikali mpya ya Marekani iingie madarakani, mshauri wa masuala ya usalama wa taifa amelazimishwa kujiuzulu na mwingine aliyependekezwa kuchukua nafasi hiyo muhimu kukataa pendekezo hilo. Baada ya kujiuzulu Michael Flynn kutokana na tuhuma za kuwa na mawasiliano ya karibu na Warussia, Rais Donald Trump alimuarifisha Robert Harward kuwa mshauri mpya wa usalama wa taifa wa nchi hiyo. Pamoja na hayo lakini jenerali huyo mstaafu hakuwa tayari kushirikiana na serikali ya Trump. Licha ya White House kudai kwamba Robert Harward alikataa ombi hilo kutokana na sababu za kifamilia lakini wajuzi wa mambo wanasema kuwa jenerali huyo mstaafu alikataa ombi hilo kutokana na hitalafu kubwa za mitazamo zilizopo baina yake na washauri wa karibu wa Trump.
Michael Flynn, Mshauri aliyejiuzulu wa Usalama wa Taifa wa Marekani
Inasemekana kuwa Harward alikusudia kuipa makao timu yake ya masuala ya usalama wa taifa katika majengo ya White House jambo ambalo lilipingwa vikali na watu walio na ushawishi katika ikulu hiyo. Inasemekana kuwa sisitizo la White House la kuendelea kulinda nafasi za wasaidizi wa Flynn ni moja ya mambo yaliyozua hitilafu hizo. Wakati huohuo inasemekana kwamba uingiliaji wa mara kwa mara wa Stephen Kevin Bannon, mwanastratejia mkuu wa Trump katika masuala ya uendeshaji wa Baraza la Usalama wa Taifa la Marekani ni moja ya sababu ambazo zimempelekea Harward kukataa nafasi ya kusimamia masuala ya usalama wa taifa. Hali ni mbaya kiasia kwamba hata baadhi ya ripoti zinasema kwamba Flynn alilazimishwa kujiuzulu si kutokana na mawasiliano yake na maafisa wa Russia bali kwa sababu ya vita vya ndani katika Baraza la Usalama wa Kitaifa ambavyo vimetokana na mabadiliko makubwa ambayo yamefanywa kwenye baraza hilo na Rais Trump. Kabla ya kuingia White House Trump alikuwa na ugomvi mkubwa na vyombo vya upelelezi na usalama vya nchi hiyo.
Robert Harwad, aliyekataa ombi la Rais Trump la kuchukua nafasi ya Flynn
Akiwa rais mteule wa Marekani, alipinga ripoti muhimu zilizoonyesha kuwa Warussia waliathiri mkondo wa uchaguzi wa hivi karibuni wa nchi hiyo na kutumia maneneo makali na ya dharau dhidi ya viongozi wa jamii ya wanahabari wa masuala ya usalama wa Marekani, jambo ambalo liliamsha wimbi la hasira na ukosoaji dhidi ya rais huyo. Hata baada ya kuingia ikulu ukosoaji huo bado haujapungua bali umeongezeka na kuchukua sura mpya. Uingiliaji wa Bannon ambaye ana misimamo mikali na ya kibaguzi ya mrengo wa kulia katika Baraza la Usalama wa Taifa umezidisha mivutano katika bara hilo na hata kupelekea baadhi ya ripoti za siri kuvuja na kuenea kwenye vyombo vya habari. Suala hilo limempelekea Rais Trump kuvituhumu vyombo vya habari za siri na usalama vya Marekani kuwa ndivyo vimekuwa vikivujisha habari hizo.
CIA, moja ya mashirika ya ujasusi ya Marekani yanayodaiwa kuvujisha habari za usalama na Rais Trump
Katika hali hiyo ya kuwepo mvutano kati ya Rais Trump na vyombo vya habari za siri na usalama vya Marekani ni wazi kuwa juhudi za rais huyo za kujaribu kumketisha Bannon kwenye kiti kilichoachwa wazi na Flynn zitakabiliwa na upinzani mkubwa wa mahasimu wa Bannon. Hii ni katika hali ambayo serikali ya Trump ndio kwanza imeanza shughuli za kuandaa sera za nje na masuala ya usalama za nchi hiyo. Mshauri wa Usalama wa Taifa wa Marekani ana jukumu muhimu la kuratibu shughuli za vyombo vilivyo chini yake katika masuala ya siasa za nje, ulinzi na usalama wa Marekani na kwa msingi huo kutokuwepo kwake tena katika mazingira haya ambapo viongozi wa nchi hiyo wanakabiliwa na kashfa na matatizo makubwa ya kiuongozi kutatoa pigo kubwa kwa uwezo, nguvu na hadhi ya Marekani dunaini.

0 comments: