OMBI LA BURUNDI KWA SERIKALI YA TANZANIA LA KUWAKAMATA WAPINZANI WAKE

Katika hali ambayo juhudi za kuondokana na mgogoro wa kisiasa nchini Burundi bado zinaendelea, serikali ya Bujumbura imeiomba Tanzania kuwatia mbaroni wapinzani wake ambao wanaosakwa na mahakama za nchi hiyo, ambao kwa hivi sasa wako kaskazini mwa Tanzania.
Bernard Ntahiraja, naibu wa Alain-Aimé Nyamitwe, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Burundi amesema kuwa baadhi ya watuhumiwa wa jaribio la mapinduzi ya kijeshi, walishiriki katika mazungumzo ya amani yaliyofanyika mjini Arusha Tanzania kati ya tarehe 16 na 18 za mwezi huu, kwa lengo la kuupatia ufumbuzi mgogoro wa nchi hiyo. Hii ni katika hali ambayo Jumatano iliyopita, Philippe Nzobonariba, Msemaji wa Serikali ya Burundi alitangaza kuwa serikali ya Bujumbura haingeshiriki mazungumzo hayo kutokana na kile alichosema ni ushiriki wa wapinzani walioshiriki katika jaribio la mapinduzi ya kijeshi dhidi ya Rais Pierre Nkurunziza. Ususiaji wa mazungumzo hayo na serikali ya Burundi umejiri katika hali ambayo licha ya kupita mwaka mmoja tangu Rais Nkurunziza ashiriki uchaguzi wa rais kwa muhula wa tatu na kuibuka mshindi, bado mgogoro wa kisiasa nchini Burundi unaendelea kushuhudiwa. Wapinzani waliitaja hatua ya rais huyo ya kugombea tena uchaguzi wa rais uliopita kuwa ni kinyume cha katiba na makubaliano ya Arusha, ambayo yalihitimisha vita vya ndani nchini Burundi.
Rais Pierre Nkurunziza wa Burundi
Katika kipindi hiki chote mgogoro wa kisiasa umezidi kushtadi nchini Burundi huku anga ya kisiasa ikizidi kuharibika. Mauaji ya kuvizia, kamatakamata vitendo vya ukatili na ukandamizaji dhidi ya wapinzani ni miongoni mwa mambo ambayo yameshuhudiwa nchini humo katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita. Vitendo hivyo vimeifanya jamii ya kimataifa kupiga makelele, huku viongozi wa serikali ya Bujumbura  wakikana katakata tuhuma hizo wanazoelekekezewa. Licha ya juhudi kubwa za viongozi wa kieneo kufanyika kupitia upatanishi wa Uganda na Tanzania kwa ajili ya kuupatia ufumbuzi mgogoro wa kisiasa wa nchi hiyo, lakini bado viongozi wa chama tawala cha CNDD-FDD na Rais Pierre Nkurunziza wamekataa kukubaliana na upatanishi huo. Hii ni katika hali ambayo Rais Nkurunziza amekataa kuwafungulia njia maripota wa haki za binaadamu kuingia nchini humo. Katika mazingira hayo, mkwamo wa kisiasa nchini Burundi umezidi kupanuka huku rais huyo akitumia mkono wa chuma kukabiliana na wapinzani. Katika fremu hiyo, Rais Nkurunziza amekanusha tuhuma za kuhusika kwake na mchafukoge na kuzituhumu pande kadhaa ikiwemo Rwanda kuwa zinaingilia masuala ya ndani ya Burundi kwa kuchochea wapinzani na kuwapatia silaha kwa ajili ya kuchafua usalama nchini humo, tuhuma ambazo viongozi wa nchi jirani hususan Rwanda wamekuwa wakizikadhibisha vikali. Hivi sasa na kwa mara nyingine wapinzani wamekutana nchini Tanzania na kuitaka serikali ya Bujumbura kushiriki mazungumzo ya amani ya mjini Arusha kwa ajili ya kujadili matatizo ya kisiasa yanayoikabili nchi yao.
António Manuel de Oliveira Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa
Pamoja na hayo si tu kwamba viongozi wa serikali wamekataa kushiriki mazungumzo hayo, bali wameitaka serikali ya Tanzania kuwatia mbaroni wapinzani hao na kisha kuwakabidhi kwa serikali ya Bujumbura. Kabla ya hapo António Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa alitangaza kuwa kumaliza mgogoro wa sasa nchini Burundi ni kati ya mambo yatakayopewa kipaumbele katika utendajikazi wake. Hata hivyo inaonekana kuwa viongozi wa chama tawala na rais wa nchi hiyo mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, hawajafungua mlango kwa ajili ya kufanyika upatanishi na kutatuliwa mzozo uliopo. Hii ni katika hali ambayo taifa hilo lina kumbukumbu ya kushuhudia vita vya ndani vya kutisha ambavyo vilisababisha maafa ya maelfu ya watu, ambapo kumetanda hali ya wasi wasi wa kuibuka tena moto wa vita vingine kama hivyo. Pamoja na hayo hivi sasa Rais Pierre Nkurunziza kwa kutumia jeshi anawakandamiza wapinzani wake ambapo matokeo yake ni kupanuka ukandamizaji huo hadi nje ya mipaka ya nchi hiyo.

0 comments: