MSHAURI WA TRUM KUHUSU USALAMA AJIUZULU

Mshauri mkuu wa rais Donald Trump amejiuzulu baada ya kukabiliwa na kushfa ya udanganyifu, kuhusiana na mazungumzo aliyoyafanya na balozi wa Urusi. Ikulu ya White House imekwishatangaza atakayekaimu katika nafasi hiyo.
USA Michael Flynn in Washington (Reuters/Y. Gripas) Michael Flynn, mshauri mkuu wa Rais Trump kuhusu masuala ya usalama ambaye amejuzulu
Mshauri huyo, Michael Flynn hapo awali alikuwa amekanusha kuhusisha suala la vikwazo dhidi ya Urusi, katika mazungumzo na balozi wa Urusi nchini Marekani Sergei Kislyak, wakati ambapo alikuwa hajaanza rasmi majukumu yake.
Hili linachukuliwa kama pigo kubwa kwa utawala wa Donald Trump ambao haujadumu hata kwa kipindi cha mwezi mmoja. Kwa siku kadhaa uvumi umekuwa ukienea, kwamba Flynn ambaye ni Jenerali mstaafu, alimdanganya Makamu Rais Mike Pence, ambaye alijitokeza hadharani kumtetea.
Katika barua yake ya kujiuzulu, Flynn amesema ''bila kukusudia'' alimpa Makamu Rais ''taarifa ambazo sio kamilifu'' kuhusu mazungumzo yake ya simu na balozi  Kislyak wa Urusi.
Ikulu ya White House mjini Washington imesema imemteuwa Luteni Jenerali Joseph Kellogg ambaye amekuwa mwenyekiti wa baraza la majenerali, kukaimu katika nafasi iliyoachwa wazi na Michael Flynn. Vyombo vya habari nchini Marekani viliripoti jana Jumatatu, kwamba utawala wa Donald Trump ulikwishatahadharishwa mapema mwaka huu kuhusu mahusiano kati ya Michael Flynn na Urusi.
Mwanzo wa maswali magumu
Maswali sasa yanaanza kuulizwa kuhusu watu katika utawala wa Marekani ambao walijua kuwepo kwa mazungumzo hayo, na kwa nini Rais Trump hakuchukua hatu mapema kumvua Flynn majukumu yake.
USA Donald Trump und Michael Flynn in Palm Beach (Reuters/C. Barria) Msemaji wa Ikulu ya Washington amesema Rais Trump hakujua chochote kuhusu udanganyifu wa Michael Flynn
Kabla ya Michael Flynn kuwasilisha barua yake ya kujiuzulu, msemaji wa Ikulu ya White House  Sean Spencer alisisitiza kuwa Rais Trump  hakufahamishwa chochote kuhusU mazungumzo kati ya Michael Flynn  na balozi wa Urusi kuhusu vikwazo ilivyowekewa nchi hiyo.
Yeyote atakayechukua nafasi ya Flynn ataliongoza Baraza la Usalama wa Taifa mnamo wakati utawala mchanga wa Rais Trump ukikabiliana na changamoto kubwa, likiwemo jaribio la hivi karibuni la makombora ya kivita lililofanywa na Korea Kaskazini.
Vile vile utawala wa Trump unaogelea katika dimbwi la msukosuko uliotokana na amri ya rais huyo kuwapiga marufuku kuingia Marekani, watu wote kutoka mataifa saba yenye waislamu wengi, amri ambayo hivi sasa imesimamishwa na mahakama.
Michael Flynn ambaye alikuwa muungaji mkubwa wa Donald Trump tangu hatua za awali za kampeni yake, amekuwa akihimiza msimamo mkali dhidi ya Iran na kulegeza sera dhidi ya Urusi, mtazamo ambao ni kunyume kabisa na ule wa utawala uliotangulia wa Rais Barack Obama.

0 comments: