GARI LA MBUNGE LAUA, MWENYEWE ANUSURIKA


Mtumishi wa Hospitali ya Wilaya ya Magu mkoani Mwanza, Moses Mjuni amefariki dunia baada ya kugongwa na gari la Mbunge wa Tarime Mjini (Chadema), Esther Matiko katika Kijiji cha Kishamba wilayani humo.Mkuu wa Wilaya ya Magu, Khadija Nyembo alisema jana kwamba ajali hiyo ilitokea juzi saa mbili usiku, “Gari la mbunge lilimgonga mtumishi wetu wa Hospitali ya Magu ambaye alikuwa anaendesha pikipiki na dereva wa gari hilo amekamatwa yupo polisi,” alisema Nyembo.
Akizungumza kwa simu jana, Matiko alisema ajali hiyo ilitokea takribani kilomita 10 kutoka Daraja la Mto Simiyu wakati akitoka Mwanza ambako walikutana na mwendesha pikipiki na dereva wake, Kelvin Matango alikuwa akimkwepa baada ya kuingia upande wake.
“Nilitoka Mwanza saa 12:00 jioni kwenda jimboni kwangu (Tarime), tulipopita mbele kidogo karibu kilomita 10 kutoka daraja la Mto Simiyu, ghafla alijitokeza mwendesha pikipiki akawa anaendesha kwa kuyumbayumba na dereva alishindwa jinsi ya kumkwepa akamgonga, mimi nilikuja kuona yule mtu ameshafariki dunia,” alisema Matiko.
Matiko alisema licha ya kwamba hakupata majeraha, baada ya kutokea ajali hiyo alipelekwa katika Hospitali ya CF ya jijini Mwanza ambako alipewa dawa na kuruhusiwa.
Hata hivyo, Matiko alisema alikuwa akisikia maumivu makali ya mgongo na mbavu hivyo kutakiwa kwenda kufanyiwa vipimo kuona kama atakuwa amepata madhara.
“Nasikia maumivu makali ya mgongo na mbavu za kulia, nahisi mkanda wa gari ulinibana zaidi, nilitakiwa kwenda hospitali ya CF kufanyiwa uchunguzi lakini nimeshindwa kwa sababu hapa tunapozungumza naenda Magu kumaliza masuala ya polisi kwani dereva na gari yupo polisi,” alisema Matiko.
Alisema baada ya kumaliza kushughulikia masuala hayo ndipo atarudi tena hospitali kufanya uchunguzi wa afya yake.

0 comments: