ASASI ZA KIMATAIFA ZATAHADHARISHA ONGEZEKO LA MACHAFUKO AFRIKA YA KATI

Taasisi tano za kimataifa zimetahadharisha juu ya kushadidi vitendo vya ukatili nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Asasi hizo ukiwemo Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika na Umoja wa Ulaya zimetoa ripoti ambayo pia imetiwa saini na jumuiya za kiuchumi za katikati mwa Afrika na Jumuiya ya Nchi Zinazozungumza Lugha ya Kifaransa (Francophone),  zikiyataka makundi yanayohusika katika mapigano nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati kuhitimisha hitilafu zao mara moja.
Wafuasi wa genge la kigaidi la Kikristo, Anti-Balaka
Katika ripoti hiyo taasisi hizo zimeonya pia kwamba kila shambulizi litakalowalenga raia wa kawaida, wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa na asasi za kiraia nchini humo,  litafuatiliwa kisheria katika vyombo vya mahakama. Kwa upande mwingine asasi hizo zimepongeza askari wa kofia ya buluu wa kusimamia amani wa Umoja wa Mataifa MINUSCA katika kuwalinda raia kunako hujuma za makundi ya waasi nchini humo. Aidha zimelaani vikali hujuma na uharibifu uliowakumba raia na kuwafanya kuwa wakimbizi ndani na nje ya Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Rais wa zamani wa nchi hiyo François Bozizé
Ni vyema kuashiria kwamba, Jamhuri ya Afrika ya Kati ambayo ni kati ya nchi masikini zaidi duniani, ilitumbukia katika mgogoro wa kisiasa mwaka 2013 baada ya kuondolewa madarakani rais wa zamani wa nchi hiyo François Bozizé kufuatia hujuma ya waasi wa Seleka nchini humo. Tangu wakati huo hadi sasa nchi hiyo imekuwa uwanja wa mapigano ya kila uchao kati ya makundi hasimu, hususan lile la Kikristo la Anti-Balaka na lile la Seleka.

0 comments: