AMNESTY: SERIKALI YA SYRIA IMEWANYONGA WATU 13,000

Shirika la kimkataifa la kutetea haki za binaadamu la Amnesty International limesema serikali ya Syria imewaua zaidi ya watu 13,000 tangu kuanza kwa vuguvugu la mapinduzi ya umma mwaka wa 2011
Syrien Regierungssoldat in Ost-Aleppo (Getty Images/AFP)
Katika ripoti ya utafiti uliofanywa kati ya 2011 na 2015, Amnesty International imesema kati ya watu 20-50 walinyongwa kila wiki katika gereza la Saydnaya, mauaji yaliyoidhinishwa na maafisa wa ngazi za juu serikalini, wakiwemo wasaidizi wa Rais Bashar al Assad, na kufanywa na jeshi la polisi.
Ripoti hiyo iliyataja mauaji hayo kuwa ni "kampeni iliyopangwa ya mauaji ya kinyume cha sheria”. Naibu mkurugenzi wa utafiti wa ofisi ya kikanda ya Amnesty mjini Beirut Lynn Maalouf amesema shirika hilo limeorodhesha karibu mbinu 35 tofauti za mateso nchini Syria tangu mwishoni mwa miaka ya 80, vitendo ambavyo vimeongezeka tangu mwaka wa 2011. "Amnesty international inafichua kampeni ya mpangilio ya mauaji ya kinyume cha sheria kwa njia kuwanyonga watu wengi kila wiki, yanayofanywa Jumatatu na Jumatano. Kati ya watu 20 na 50, hutolewa kwenye vyumba vyao, na kupelekwa katika jumba jingine mjini Sednaya na kunyongwa".
Syrien Lynn Maalouf | Massenhinrichtungen (picture alliance/AP Photo/B. Hussein)
Mashirika mengine ya haki za binaadamu yamepata ushahidi wa mateso makubwa yaliyosababisha vifo katika magereza ya Syria: katika ripoti yake mwaka jana, Amnesty iligundua kuwa zaidi ya watu 17,000 waliuawa kwa kuteswa wakatiwa kizuizini kote Syria tangu mwaka wa 2011, ikiwa ni kiwango cha wastani cha zaidi ya watu 300 kwa mwezi. Takwimu hizo zinaweza kulinganishwa na vifo vilivyotokea katika viwanja vya mapambano vya Aleppo, mojawapo ya maeneo makali ya vita nchini Syria, ambako watu 21,000 waliuawa kote mkoani humo tangu 2011. Maalouf anasema hakuna sababu ya kuamini kuwa dhuluma hizo zimekomeshwa tangu mwaka wa 2015, maana huenda maelfu ya watu wameuawa.
Ameongeza kuwa mauaji haya hufanyika baada ya kuendeshwa kesi ya uongo inayodumu dakika moja au mbili, lakini yanaidhinishwa na maafisa wakuu akiwemo Mufti mkuu, na waziri wa ulinzi. Maalouf ametoa wito wa kuchunguzwa madai hayo "Tunatoa mwito kwa Umoja wa Mataifa kuanzisha uchunguzi wa huru na wazi kuhusu kinachotokea Sednaya na kwa hili kufanyika katika njia ya mafanikio, tunaitaka serikali ya Syria kuwaruhusu waangalizi wake, waangalizi wa Umoja wa Mataifa ambao wako huru, kuingia Sednaya, lakini pia katika magereza yote na vituo vya kuwazuilia watu kote Syria".
Huwa nadra kwa maafisa wa serikali ya Syria kuzungumzia madai haya ya mateso na mauaji ya watu wengi. Katika siku za nyuma, walipinga ripoti za mauaji ya kikatili yaliyoorodheshwa na mashirika ya kimataifa ya haki za binaadamu, wakiritaja kuwa ni propaganda. Matokeo ya ripoti iliyotolewa leo yalitokana na mahojiano yaliyofanyiwa wafungwa wa zamani 31 na maafisa wengine 50 na watalaamu, wakiwemo walinzi wa zamani wa magereza na majaji.

0 comments: