AFGHANISTAN: MAMIA YA WANAWAKE WATUMWA MWA NGONO NA KUNDI LA ISIS NCHINI HUMO

Mkuu wa Taasisi ya 'Uadilifu kwa ajili ya Wote' nchini Afghanistan amesema kuwa, kundi la kigaidi na ukufurishaji la Daesh limewafanya watumwa wa ngono zaidi ya wanawake 100 katika miji tofauti ya mkoa wa Nangarhar nchini humo ndani ya kipindi cha miaka miwili iliyopita.
Hamideh Wardak, ameyasema hayo katika kikao na waandishi wa habari mjini Kabul, mji mkuu wa Afghanistan na kuongeza kuwa, wanawake hao walitiwa mbaroni na kundi hilo katika miji ya Kut na Haskeh Mineh Achin na kisha kufanywa watumwa wa ngono. Ameongeza kuwa, wanawake wengi walikamatwa katika mji wa Achin ambao ni makao makuu ya genge hilo nchini Afghanistan.
Uhalisia wa genge la ISIS katika kuwafanya watumwa wa ngono wanawake
Aidha ameelezea ongezeko la vitendo vya ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na kusema kuwa, kwa mujibu wa ripoti zilizotolewa hivi karibuni, jumla ya kesi 35 zimeripotiwa katika mji wa Herat tangu mwanzoni mwa mwaka huu pekee. Mkuu wa Taasisi ya 'Uadilifu kwa ajili ya Wote' nchini Afghanistan amesema kuwa siku chache zilizopita, mwanamke mmoja alimwagiwa tindikali katika eneo la Bagh Bala mjini Kabul, huku wanawake wengine wawili wakichomwa moto katika mkoa wa Nangarhar. 
Wanawake wa Afghanistan wakionyesha machungu yao
Kwa mujibu wa Hamideh Wardak, mwanamke mmoja ameripotiwa kufariki dunia kwa kuchapwa bakora katika mkoa wa Urozgan kwa tuhuma za kukimbia kuolewa na wanachama wa kundi hilo, na kwamba hayo ni matukio machache sana yanayowakabili wanawake wa Afghanistan kipindi hiki. Kadhalika amesema kuwa siku chache zilizopita wanawake wawili walishikwa na wanachama wa kundi la Taleban katika mji wa Day Mirdad mkoa wa Maidan Wardak, na kwamba wanachama hao wanataka kuwaoza kwa nguvu kwa kile kinachoitwa Jihadun-Nikaah.
Magaidi wakufurishaji wa Daesh nchini Afghanistan
Kwa ajili hiyo Hamideh Wardak ameitaka serikali ya Afghanistan kuzuia mwendelezo wa jinai za makundi hayo ya kigaidi dhidi ya wanawake na kwamba kuendelea kimya cha serikali ni sawa na kufungua njia ya mwendelezo wa ukatili na jinai hizo

0 comments: