WABUNGE WA REPUBLICAN WAMTAKA TRUMP AUHAMISHE QUDS UBALOZI WA MAREKANI ISRAEL

Wabunge wa chama cha Republican katika bunge la Marekani wanaandaa barua ya kumpelekea rais mteule wa nchi hiyo Donald Trump wakitaka serikali mpya ijayo ichukue hatua haraka ya kuuhamishia Baitul Muqaddas ubalozi wa nchi hiyo ulioko Tel Aviv.
Barua hiyo hadi sasa imeshasainiwa na wabunge 100 wa chama cha Republican katika Bunge la Wawakilishi huku ikiendelea kusambazwa ili kupata idadi kubwa zaidi ya watakaoisaini.
Sehemu moja ya barua hiyo inamtaka Tump kuchukua hatua ya haraka mara baada ya kushika hatamu za uongozi ya kuuhamishia Quds tukufu inayokaliwa kwa mabavu ubalozi wa Marekani ulioko Tel Aviv, mji mkuu wa utawala haramu wa Israel.
Trump (kushoto) na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu
Sehemu ya barua hiyo ya wabunge wa chama cha Republican inaeleza kuwa: "Kuuhamisha ubalozi huo kutaimarisha muungano wa kipekee uliopo baina ya Israel na Marekani na kufikisha ujumbe wa wazi kwa dunia kwamba tunaiunga mkono Israel kwa kuitambua Quds (Jerusalem) kuwa mji mkuu wake wa milele.
Msikiti mtukufu wa Al-Aqsa ulioko Quds Tukufu inayokaliwa kwa mabavu
Tarehe 5 ya mwezi huu wa Januari, Jordan, ambayo inasimamia uendeshaji wa eneo la msikiti mtukufu wa Al-Aqsa katika Baitul Muqaddas Mashariki ilimtahadharisha Donald Trump juu ya matokeo ya "balaa" endapo ataamua kutekeleza ahadi aliyotoa wakati wa kampeni za uchaguzi wa rais wa Marekani ya kuuhamishia Quds tukufu inayokaliwa kwa mabavu ubalozi wa nchi hiyo ulioko Tel Aviv. Harakati ya Ukombozi wa Palestina (PLO) nayo pia imeionya Marekani juu ya hatua hiyo na kueleza kwamba balozi zote za Marekani katika Ulimwengu wa Kiarabu itapasa zifungwe kutokana na ghadhabu za wananchi wa mataifa ya Kiarabu dhidi ya hatua hiyo…/

0 comments: