UCHAGUZI MDOGO WA UBUNGE ZANZIBAR; MGOMBEA WA UPINZAMI ADAI NI 'VURUGU TUPU'

Uchaguzi mdogo wa jimbo la ubunge la Dimani viswani Zanzibar nchini Tanzania umefanyika leo huku chama kikuu cha upinzani visiwani humo cha Wananchi (CUF) kikilalamikia kile kilichodai kuwa ni ukiukaji mkubwa wa sheria na taratibu za uchaguzi.
Uchaguzi huo umefanyika kujaza nafasi iliyoachwa wazi na mbunge wa jimbo hilo kwa tiketi ya chama tawala cha Mapinduzi (CCM) Hafidh Ali Tahir aliyefariki dunia mwezi Novemba mwaka uliopita wa 2016 ulitazamiwa kushuhudia mchuano mkali baina ya mgombea wa chama hicho na yule wa CUF anayewakilisha muungano wa upinzani wa UKAWA.
Hata hivyo mapema leo Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano wa CUF Salim Bimani alivieleza vyombo vya habari kuwa daftari la wapiga kura lililotumika katika uchaguzi wa leo silo lililotumiwa katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 2015 na kwamba wapiga kura hewa wengi wamepiga kura katika uchaguzi huo kwa maslahi ya CCM.
Wakati huohuo mgombea wa ubunge wa jimbo hilo kwa tiketi ya CUF Abdulrazak Khatib Ramadhani amemwandikia barua rasmi Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Uchaguzi ya Taifa (NEC) kulalamikia kile alichodai uchaguzi wa vurugu uliofanyika leo.
Taarifa ambazo zimethibitishwa na mwandishi wa Radio Tehran zinaeleza kuwa mawakala kadhaa wa vyama vya upinzani pamoja na waandishi wa habari walitimuliwa kwenye vituo vya kupigia kura na askari wa jeshi la polisi kwa tuhuma mbalimbali.
Hadi tunaelekea mitamboni matokeo rasmi ya uchaguzi huo yalikuwa bado hayajatangazwa…/

0 comments: