SYRIA YAAPA KULIPIZA KISASI SHAMBULIO LA ISRAEL DHIDI YA UWANJA WA NDEGE WA MEZZAH

Jeshi la Syria limetangaza kuwa utawala wa kizayuni wa Israel umeshambulia uwanja wa ndege wa kijeshi wa Mezzah ulioko magharibi mwa mji wa Damascus na kuutahadharisha utawala huo kuhusu taathira mbaya za shambulizi hilo.
Taarifa ya jeshi la Syria imesema uwanja huo wa ndege wa kijeshi umeshambuliwa kwa maroketi kadhaa usiku wa kuamkia leo na kusisitiza kwamba, Syria italipiza kisasi shambulizi hilo.
Taarifa hiyo imesema, shambulizi la Israel dhidi ya uwanja wa ndege wa kijeshi wa Mezzah ni jaribio la utawala huo ghasibu la kutaka kuyasaidia makundi ya kigaidi yanayoelekea kusambaratika na kwamba Damascus itaendeleza mapambano na vita hadi ugaidi utakapotokomezwa kikamilifu nchini humo. 
Jeshi la Syria likiendela kuwasaka wapiganaji wa Daesh, Aleppo
Ripoti zinasema shambulizi hilo la Israel lililenga maghala ya mafuta yanayotumiwa na kikosi maalumu cha jeshi la Syria cha Republican Guards.
Israel inahesabiwa kuwa miongoni mwa pande zinazoyasaidia na kuyaunga mkono makundi ya kigaidi nchini Syria hususan kundi la magaidi wa Daesh.

0 comments: