WAUMINI wa dini ya kiislam mkoani Kigoma wameaswa wasitumie kitabu cha dini(QUR`AN) kuleta mifarakano katika jamii ili,kutimiza utashi wenye maslai ya kuigawa dini hiyo katika makundimakundi,badala yake waijenge dini kwa mshikamano wenye tija kwa umati wa Mtume Muhamad( SWA).
Akitoa kauli hiyo mbele ya umati wa waumini hao hivikaribuni Kigoma Ujiji mkoani humo,kwenye madhimisho ya sherehe za Kuzaliwa kwa Mtume huyo,Shekhe Mkuu wa wilaya Kigoma,Alhaji Twalha Kiburwa alisema maadhimisho hayo yameratibiwa na Jumuia ya Shia Ithnaasheri.
Alieleza kuwa,siku za hivi karibuni kuna baadhi ya waislam wamejiingiza katika migongano ya wenyewe kwa wenyewe inayochangia ubaguzi baina yao,ambapo wanaofanya hivyo wanafanya kwa maslahi binafsi kwa kutumia aya na hadithi kadhaa katika vitabu vya dini kwa kujenga fitina zao.
Alifafanua kuwa,tofauti ya madhehebu miongoni mwa waislam siyo kigezo cha dhehebu moja kujiona ni bora zaidi ya dhehebu linguine,kilichopo ni kuzingatia misingi ya Uislamu na si tofauti za madhehebu kwa kuwa hazina tija katika misingi ya kuwafanya wasiungane katika kuiendeleza dini.
Naye Mwenyekiti wa Bara la Afrika wa Taasisi ya Bilal Muslim, Muslim Abdallah Sheni amewakumbusha waumini wa dini hiyo wazingatie misingi ya dini inayowajenga kuwa na upendo, amani na mshikamano ,badala ya kila mtu kufanya maelekezo ya dhehebu lake kuwa ndiyo msingi mkuu wa dini hiyo.
Sheni alisema hawana budi kushirikiana katika kuitumikia jamii ikiwemo kupeleka miradi mbalimbali ya kijamii hasa huduma ya Afya,maji na nyinginezo, kwa kutumia taasisi zao,ili kuimarisha mahaba kwa dini hiyo ,kwa kila mwanajamii.
Kwa upande wa Mwenyekiti wa Taasisi ya Bilal Muslim Mission mkoani Kigoma,Sheikh Abdulwahid Abayat alisema ili kurudisha umoja miongoni mwao hawana budi kuwajengea watoto misingi ya dini kwa kuwafundisha matendo mema kwa kuwa wakarimu,wenye upendo na kumpenda kila mtu.
Shekhe Abayat alisema changamoto ya kufarakanamiongoni mwa dini hiyo,inachangiwa na kutoandaliwa vyema katika misingi stahiki ya imani juu watoto wa kiislam ikiwemo maisha ya kumcha mungu ambapo ni silaha kwa jamii kuishi kwa amani na upendo
0 comments: