SERIKALI YAWAONDOA HOFU WANANCHI JUU YA HALI YA UPATIKANAJI WA CHAKULA NCHINI.

HOFU
Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi Dkt. Charles Tizeba akizungumza na waandishi wa habari kuhusu hali ya upatikanaji wa chakula nchini jana jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Mhandisi Mathew Mtigumwe.
HOFU 2
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini wa Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi akitoa maelekezo kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati wa mkutano wa Waziri wa Wizara hiyo Dkt. Charles Tizeba9hayupo pichani) na waandishi hao kuhusu hali ya upatikanaji wa chakula nchini jana jijini Dar es Salaam.
HOFU 3
Baadhi ya waandishi wa habari wakifuatilia mkutano baina yao na Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi Dkt. Charles Tizeba (hayupo pichani) kuhusu hali ya upatikanaji wa chakula nchini, mkutano umefanyika katika ukumbi wa mikutano wa Wizara hiyo jana jijini Dar es Salaam. (Picha zote na: Frank Shija – MAELEZO.)

Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO.

SERIKALI imesema kuwa hali ya upatikanaji wa chakula nchini ni ya kuridhisha na kuwataka wananchi kupuuza taarifa zinazodai kuwa hali ya chakula ni mbaya.
Hayo yamebainishwa jana jijini Dar es Salaam na Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi Dkt. Charles Tizeba wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu hali ya upatikanaji na chakula nchini.
“Ndugu waandishi ukweli ni kwamba hali ya upatikanaji wa chakula nchini ni ya kuridhisha sana katika maeneo mengi, hivyo siyo kweli kwamba kuna tatizo la njaa kama baadhi ya watu wanavyojaribu kupotosha,” alisisitiza Dkt. Tizeba.
Aidha Dkt. Tizeba aliongeza kuwa pamoja na kuwepo kwa hali nzuri ya chakula, Serikali kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) imeendelea kuweka akiba ya chakula kwa kununua jumla ya tani 62,087.997 za mahindi ili kuhakikisha nchi inaendelea kuwa na chakula cha kutosha,
Dkt. Tizeba amesema kuwa kwa mwaka wa fedha 2016/2017 Serikali  imejipanga kununua jumla ya tani 100,000 za chakula ambapo hadi  kufikia Januari 8 mwaka 2017 imenunua jumla ya tani 62,087.997 za mahindi sawa na asilimia 62 ya lengo ililojiwekea.
“Kati ya kiasi kilichonunuliwa, tani 38,162.280 zimenunuliwa kupitia vituo vya ununuzi na tani 23,925.717 kupitia vikundi vya wakulima hivyo hadi kufikia tarehe 12 Januari, 2017 Wakala wana akiba ya tani 88,152.443 za mahindi,” alisema Dkt. Tizeba.
Waziri Tizeba ameongeza kuwa hadi kufikia katikati ya mwezi Januari, 2017 hali ya chakula na upatikanaji wake hapa nchini bado ni ya kuridhisha na hasa upatikanaji wa vyakula kama mchele na maharage ikilinganishwa na zao la mahindi.
Aidha, Wizara kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI, FAO, TFNC pamoja na wadau wengine wanaendelea kufanya tathmini ya kina ya hali ya chakula na lishe nchini ambayo inatarajiwa kukamilika Januari 28 mwaka 2017 na itazihusisha Halmashauri 55, tathmini hiyo itaiwezesha Serikali kupata taarifa za uhakika zaidi kuhusu hali ya chakula na lishe nchini.
Amefafanua kuwa kutokana na hali ya mwenendo wa unyeshaji wa mvua za vuli na msimu kutokuridhisha katika maeneo mengi ya nchi, Serikali imewashauri wakulima kutumia mbegu zitakazokomaa mapema na kupanda mazao yanayostahimili ukame pamoja na kutumia kwa uangalifu na kuhifadhi akiba ya chakula cha kutosha kwa matumizi katika kaya.
Aidha, Sekta binafsi zimehamasishwa kuendelea kushiriki katika kutoa masoko ya kununua na kuuza mazao katika maeneo yenye ziada na kuyauza katika maeneo yenye uhaba.
Ufafanuzi huo umetolewa kufuatia kuwepo kwa taarifa za upotoshwaji juu ya hali ya upatikanaji wa chakula hapa nchini ambapo Dkt. Tizeba amesema huo ni upotoshaji wenye lengo la kuwatia hofu wananchi.

0 comments: