RAIS MPYA WA GAMBIA AAPISHWA; JAMMEH ANG'ANGA'ANIA MADARAKANI

Adama Barrow ameapishwa na kuwa Rais mpya wa Gambia huku Yahya Jammeh aliyetawala nchi hiyo kwa miaka 22 aking'ang'ania madaraka ya nchi.
Baadhi ya duru zinasema kuwa Barrow ameapishwa leo kuwa rais mpya na wanajeshi wa nchi za Afrika Magharibi wako tayari kuingilia kati. Sherehe za kuapishwa Adama Barrow zimefanyika nje ya nchi katika ubalozi wa Gambia nchini Senegal.
Hayo yanajiri katika hali ambayo, mawaziri na viongozi mbalimbali wa serikali ya Rais Jammeh wameendelea kujiuzulu na hivyo kuzidi kumdhoofisha kiongozi huyo mwenye nia ya kung'ang'ania madaraka.
Makamu wa rais nchini Gambia Isatou Njie-Saidy amejiuzulu saa chache kabla ya muda wake wa kuongoza kutimia. Asidha Waziri wa Mazingira na Elimu ya Juu pia amejiuzulu, ikiwa ni msururu wa mawaziri kumtoroka Jammeh kufuatia hatua yake ya kukataa kujiuzulu baada ya zaidi ya miongo miwili ya utawala.
Adama Barrow, Rais mpya wa Gambia
Wakati huo huo, majeshi ya mataifa ya magharibi mwa Afrika yanatarajiwa kuingia nchini Gambia leo ili kuhimiza uhamisho wa mamlaka. Baadhi ya ripoti ambazo hazijathibitishwa zinasema kuwa, vikosi vya Senegal tayari vimeingia nchini Gambia.
Katika upande mwingine Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilitazamiwa kufanya mkutano wa dharura hii leo kuhusiana na mgogoro wa kisiasa na kunukia machafuko ya umwagikaji damu nchini Gambia.
Rais Yahya Jammeh ambaye alikuwa amekubali kushindwa na Adama Barrow katika uchaguzi wa rais uliofanyika mwezi Desemba na hata kumpongeza mpinzani wake huyo, ghafla alibadilisha uamuzi na kuyakataa matokeo kwa madai kuwa zoezi la uchaguzi lilitawaliwa na dosari nyingi na sasa anataka uchaguzi wa rais ufanyike tena.

0 comments: