MIAKA 53 YA MAPINDUZI “WAZO LA DKT MOHAMMED SEIF KHATIB KUANZISHA MAKUMBUSHO YA MAPINDUZI YA ZANZIBAR LIFANYIWE KAZI”

Na Judith Mhina – MAELEZO

“Wakati umefika wa kujenga makumbusho ya Taifa ya Mapinduzi ya Zanzibar, ili kizazi cha sasa na kijacho waweze kujifunza na kuipitia historia muhimu kwa Watanzania na wageni kutoka nje. 

Hayo ni maneno ya msingi ambayo yamesemwa na Dkt Mohammed Seif Khatibu wakati wa mahojianno yake na Idara ya Habari MAELEZO mapema mwishoni mwa wiki.
Dkt Khatib alisisitiza “Ni vema kuonesha katika picha, maandishi na sura halisi za historia ya Zanzibar kabla yaani wakati wa Waajemi, Wareno, Waarabu, Waingereza na sasa Serikali ya Mapinduzi”. 

Dhamira ya makumbusho hayo, Dkt. Khatib amesema “Vijana wengi ukiwaambia nchi hii kulikuwa na unyanyasaji wa Waafrika hawakubali maana hawajui historia, waelezwe kwa nini tuko huru, kuna wasioitakia mema Zanzibar wanapotosha historia hiyo”.

Kumbe kwa kuweka makumbusho na usahihi wa historia ya nyuma kabla, wakati, baada ya Mapinduzi na yanayotokea sasa, hayo yote yakiwa katika makumbusho yatakuwa msingi wa historia ya Zanzibar hatua ambayo itasaidia kuwekwa wazi mambo yaliyowahi kutokea, hivyo sio rahisi kwa mtu yoyote ambaye ana agenda ya kupotosha umma kufanya hivyo. 

Lakini kwa sasa ni kweli kabisa mtu yoyote anaweza akasema vyovyote atakavyo kwa kuwa hawajui historia na wala hawana mahali pa kurejea historia ya Mapinduzi ya Zanzibar.
“Watu walitoka Kongo, Malawi, Kigoma na Tabora wakibebeshwa pembe za Ndovu na kusafiri kwa mguu,  wakifuata njia ya reli ya kati, mpaka Bagamoyo na  kusafirishwa na boti mpaka Unguja na kuwekwa sokoni kuuzwa kama samaki katika soko la watumwa. Huu ndio ukweli” alisema Dkt Khatib.

Tuchukulie mfano wa jirani zetu Rwanda walikubwa na mauaji yakimbari mwaka 1994, kwa kutambua kuwa hicho siyo kitu kizuri kutokea tena hapa duniani wameona waweke makumbusho ya kitaifa. Inahuzunisha lakini ndio ukweli, unapoona yale mafuvu ya vichwa yalivyopangwa huwezi kuamini kama hiyo ni hali halisi iliyotokea hapa duniani.
Kwa Wanyarwanda na watu wengine duniani, makumbusho kimbari ni sehemu ya Utalii ikizingatia msemo wa waswahili wanasema kuona ni kuamini.

Siyo hiyo, tu hata kule Namibia kuna jumba la makumbusho la mauaji yaliyofanywa na wajerumani kwa kabila la Waherero waliuwawa katika vita ya kwanza ya dunia. Takribani Waherero nusu ya milioni waliuwawa na hivi karibuni Waherero wa Namibia walikuwa wanaomba fidia kwa Serikali ya Ujerumani, ingawa Ujerumani wameomba msamaha kwa mauaji hayo ya kimbari.

Uingereza ni nchi inayoongoza duniani kwa kuweka kumbukumbu zake katika makumbusho za Kifalme, Kimataifa, Kitaifa, Vita, Silaha, Bahari, Mtu Binafsi, Jiji au Mji husika. Uingereza ina zaidi ya makumbusho 55 ambayo yanafahamika duniani.  Mfano  “British Museum London, Natural History Museum London, National Gallery London, Science Museum London, Victoria and Albert Museum, National Maritime Museum, Museum of London City, National Portrait Gallery, National Army Museum,  Sir Johns Soanes Museum, Wallace Collection London, National War Museum nk”

Hivyo, tuunge mkono wazo hilo na tushirikiane wote kama Watanzania kuhakikisha kituo hicho cha makumbusho kinajengwa na kuhifadhi kila kinachohitajika ili kukamilisha historia husika. 

Kujengwa kwa kituo cha makumbusho Zanzibar kitasaidia kuingizia fedha kama sehemu ya Utalii wa historia ambapo mtu anayehitaji kuijua historia hiyo atapata kila kitu mahala pamoja bila kusumbuka.  Mungu ibariki Tanzania “MAPINDUZI DAIMA”.

0 comments: