CUF YALALAMIKIA 'WIZI' WA RUZUKU YAKE ; YAMTAKA RAIS MAGUFULI ACHUKUWE HATUA

Chama cha Wananchi (CUF) nchini Tanzania kimedai kuwa kimeibiwa fedha zake za Ruzuku kiasi cha shilingi milioni 369.
Akizungumza mbele ya waandishi wa habari hii leo, Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi wa chama hicho Julius Mtatiro amesema fedha hizo zilitoroshwa kutoka Hazina ya Serikali Kuu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania siku ya Alhamisi, tarehe 5 ya mwezi huu wa Januari na kuingizwa kwenye akaunti ya Benki ya NMB Tawi la Temeke, mjini Dar es Salaam.
Kwa mujibu Mtatiro, fedha hizo zimehamishiwa kwenye akaunti ya mtu binafsi aliye karibu na Profesa Ibrahim Lipumba, Mwenyekiti taifa wa CUF anayetambuliwa na Msajili wa Vyama vya Siasa.
Amesema CUF imeshangazwa na hatua hiyo kwa kuzingatia kuwa Msajili wa Vyama vya Siasa Jaji Francis Mutungi alikiandikia barua chama hicho kukitaarifu uamuzi wake wa kusimamisha mgao wake wa ruzuku kutokana na mgogoro wa uongozi uliopo mpaka chama hicho kitakaporejea katika hali shwari kiutendaji inayowezesha viongozi husika kusimamia matumizi ya fedha hizo ipasavyo.
Profesa Ibrahim Lipumba, mwenyekiti wa CUF anayetambuliwa na Msajili wa Vyama
Kupitia taarifa hiyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya CUF mbali na kushangazwa na hatua hiyo ya Hazina, amemtaka Rais Magufuli, Waziri Mkuu Kasimu Majaliwa, Gavana wa Benki Kuu (BOT), TAKUKURU, Ofisi ya Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali na vyombo vingine vinavyohusika, kuchukua hatua za dharura za kuokoa fedha hizo za umma ambazo amesema, zimepotezwa na watendaji wa Hazina kwa kuwa uhamishaji wake umefanyika bila ya vyombo rasmi vya uongozi vya CUF na vinayotambulika kisheria kuidhinisha suala hilo.
Chama cha CUF kimetumbukia kwenye mgogoro mkubwa wa uongozi tangu mwenyekiti wake Profesa Lipumba alipojiuzulu uongozi na kisha kubadilisha uamuzi wake huo, hatua ambayo imepingwa na vyombo vya juu vya uongozi vya chama hicho.
CUF inadai kuwa vyombo vya dola vya serikali ya chama tawala CCM vina mkono katika ''upikaji" wa mgogoro huo.

0 comments: