ALIYEKUWA WAZIRI MKUU ATEULIWA KUWA MAKAMU WA RAIS WA IVORY COAST

Rais Alassane Ouattara wa Ivory Coast amemteua aliyekuwa Waziri Mkuu Daniel Kablan Duncan kuwa Makamu wa Rais, cheo kipya ambacho kimeundwa kupitia katiba mpya ya nchi hiyo iliyopitishwa kwa Kura ya Maoni iliyofanyika mwishoni mwa mwaka jana.
Duncan, mwenye umri wa miaka 73 ambaye kitaaluma ni mchumi, amehudumu katika Benki Kuu na pia kama Waziri wa Fedha katika nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika na ni miongoni mwa washirika wa karibu na wa muda mrefu wa Rais Ouattara. Alijiuzulu wadhifa wake wa uwaziri mkuu hapo jana na kuvunja serikali ili kupisha mchakato wa utekelezaji katiba mpya.
Akihutubia bunge wakati wa kumtambulisha makamu wake, Rais wa Ivory Coast amesema Duncan ni mtu mwenye uzoefu, mtumishi mkubwa kwa serikali na ambaye ameonyesha sifa za kipekee za kishakhsia na kitaalamu alizonazo katika nyadhifa zote za juu alizowahi kushika.
Rais Ouattara (wa pili kulia) akimpongeza Makamu wa Rais Duncan
Cheo cha Umakamu wa Rais kiliingizwa katika katiba mpya ya Ivory Coast iliyopitishwa mwezi Novemba mwaka jana ili kuhakikisha upokezanaji wa madaraka unafanyika kwa amani itokeapo rais kufariki dunia au kupoteza uwezo wa kutekeleza majukumu yake wakati akiwa angali madarakani.
Wakodiva wengi pia wanaiona hatua hiyo kama wenzo wa kumwezesha rais Alassane Ouattara kuandaa mrithi wake wakati kipindi chake cha uongozi kitakapomalizika mwaka 2020…/

0 comments: