ZA KIMATAIFA: HIMAYA YA UMOJA WA MATAIFA KWA JUHUDI ZA IRAN, RUSSIA NA UTURUKI ZA KUUPATIA UFUMBUZI MGOGORO WA SYRIA
Posted by khamisimussa77@gmail.com at 8:57 PM
Staffan de Mistura, mwakilishi wa Katibu Mkuu
wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Syria amesema katika mazungumzo
yake kwa njia ya simu na Sergey Lavrov, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa
Russia kwamba, anaunga mkono juhudi za Iran, Russia na Uturuki zenye
lengo la kuupatia ufumbuzi mgogoro wa Syria.
Sergey Lavrov amesisitiza katika
mazungumzo hayo juu ya natija ya kikao cha hivi karibuni cha Moscow,
himaya na utayari wa Umoja wa Mataifa wa kusaidia kuandaa na kutekeleza
hati ya makubaliano baina ya serikali na makundi ya upinzani
yanayoipinga serikali ya Damascus kwa ajili ya kusitishwa mapigano
nchini Syria na kuanza mazungumzo ya Wasyria kwa Wasyria katika mji mkuu
wa Kazakhstan, Astana.
Katika mazungumzo ya siku moja
yaliyofanyika mjini Moscow tarehe 20 mwezi huu baina ya Mawaziri wa
Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Russia na Uturuki,
kulipasishwa taarifa ya pamoja iliyounga mkono juhudi za kuupatia
ufumbuzi mgogoro wa Syria. Aidha kutakiwa jamii ya kimataifa
kushirikiana katika vita dhidi ya ugaidi, kuhifadhiwa ardhi yote ya
Syria, kukataliwa utumiaji wa nguvu za kijeshi katika kuutafuitia
ufumbuzi mgogoro wa nchi hiyo, kutekelezwa azimio nambari 2254 la Umoja
wa Mataifa, kupelekwa misaada ya kibinadanmu kwa Wasyria na kuondolewa
raia katika maeneo yanayozingirwa na magaidi ni vipengee vingine vya
taarifa ya kikao hicho cha Moscow.
Kwa hakika matukio ya Syria katika miezi ya hivi karibuni
yamebadilisha mahesabu ya makundi ya kigaidi na waungaji mkono wao.
Katika fremu hiyo, kukombolewa mji muhimu na wa kiistartejia wa Halab
kunahesabiwa kuwa nukta muhimu ya mafanikio katika vita dhidi ya ugaidi
huko nchini Syria. Ushindi huo wa Halab unatazamwa na Iran na Russia
kuwa ni zaidi ya ushindani ulioko katika Mashariki ya Kati. Awali wakati
wa kuanza machafuko nchini Syria, serikali ya Marekani ilikuwa ikiamini
kwamba, kuangushwa serikali ya Rais Bashar al-Assad ni jambo
lisiloepukika hata kidogo. Ni kwa msingi huo ndio maana Washington kwa
utendaji huo wa upande mmoja ikaiunga mkono Saudi Arabia, Uturuki, Qatar
na makundi ya kigaidi huko Syria na ikayaimarisha na kuyapatia nguvu
kwa kuyatumia silaha.
Sera za Saudi Arabia na Qatar za kuzusha
migogoro pamoja na nafasi haribifu ya Marekani nchini Syria imepelekea
kutokea maafa makubwa katika nchi hiyo. Washauri wa ikulu ya Marekani
White House walikuwa wakidhani kwamba, kwa kuyaunga mkono makundi ya
kigaidi na kuyagawa sehemu tatu za makundi mazuri, mabaya na ya wastani
wangeweza kuhitimisha mara moja hatamu za serikali halali ya Syria chini
ya uongozi wa Rais Assad.
Hata hivyo, kwenda kombo huko kimahesabu kumekuwa na taathira hasi
mno. Kutokea maafa kama ya kuuawa kikatili wananchi wa Syria na makundi
ya kigaidi ya Daesh na Jabh'hat al-Nusra, kuzingirwa miji kadhaa na
kugeuzwa raia kuwa ngao ya kujikingia na wakati huo huo kuongezeka
wakimbizi ni matokeo ya utendaji wa kupenda vita nchini Syria ambapo
nchi kama Uturuki nayo kwa siasa zake imechangia katika hilo.
Aidha serikali ya Marekani badala ya
kurekebisha makosa yake, imeendelea kuyapatia misaada ya silaha makundi
ya kigaidi nchini Syria.
Bashar al-Ja'far balozi na mwakilishi wa kudumu wa Syria katika Umoja
wa Mataifa sambamba na kuashiria mgogoro wa kibinadamu ulioibuka nchini
Syria kutokana na kuwepo magaidi katika nchi hiyo amesema kuwa, ili
kuhitimisha mgogoro huo wa kibinadamu kuna haja ya kuweko ushirikiano na
uratibu wa kimataifa na serikali ya Syria katika uwanja wa kupambana na
ugaidi na wakati huo huo kutekelezwa maazimio ya Baraza la Usalama la
Umoja wa Mataifa katika uwanja huo.
Hapana shaka kuwa, himaya ya Umoja wa
Mataifa kwa juhudi za pamoja za Iran na Russia na matamshi ya Staffan de
Mistura, mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika masuala
ya Syria kuhusiana na mwenendo chanya wa matukio ya nchi hiyo, ni jibu
kwa propaganda na ukwamishaji mambo wa Marekani na Saudia baada ya
kukombolewa mji wa Halab na kufanyika kikao cha pande tatu huko Moscow
Russia.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments: