WAPINZANI WAPAMBANA NA POLISI JAMHURI YA KKIDEMOKRASIA YA KONGO

Maandamano ya nchi nzima huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) yamewalazimisha polisi kuingilia kati kukabiliana nayo.
Mtandao wa habari wa Africa News umeripoti habari hiyo leo na kusema kuwa, maandamano hayo yamefanyika leo kulalamikia kufungwa jela wanaharakati 15 wa kisiasa wanaoipinga serikali ya Rais Joseph Kabila. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, mahakama moja ya DRC imewahuku kifungo cha miaka mitatu jela wanaharakati 15 wa kisiasa wa nchi hiyo kwa tuhuma za kufanya uasi na kuvuruga utulivu na usalama wa umma.
Maandamano mjini Kinshasa, DRC
Ijapokuwa vyombo vya mahakama vya Kongo vimewaachilia huru wanaharakati 34 wa kisiasa kama njia ya kutuliza hali ya mambo, lakini machafuko yameongezeka kutokana na kuendelea kubakia madarakani Rais Joseph Kabila licha ya muda wake wa urais kumalizika tarehe 19 mwezi huu wa Disemba.
Duru za kuaminika zimesema kuwa, idadi ya waandamanaji waliouawa kwenye maandamano ya kupinga serikali inazidi kuongezeka na hivi sasa imeshapindukia watu 30. Ikumbukwe kuwa serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imepiga marufu maandamano nchi nzima.
Polisi wa DRC wakijiandaa kukabiliana na maandamano

Wakati huo baadhi ya duru za DRC zimetangaza kuwa, jana usiku mazungumzo baina ya serikali na wapinzani yalianza kwa upatanishi wa viongozi wa kidini wa nchi hiyo.
Rais Joseph Kabila, aliyeingia madarakani baada ya kuuliwa baba yake, Laurent Desire Kabila mwaka 2001 ameshashiriki kwenye chaguzi mbili za mwaka 2006 na 2011 na kushinda. Kwa mujibu wa Katiba ya Kongo, Joseph Kabila hana haki ya kushiriki kwenye uchaguzi mwingine baada ya kuwa Rais kwa vipindi viwili mfululizo.
Rais Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo

0 comments: