SERIKALI YA MISRIYAPITISHA MPANGO WA KUIPATIA SAUDIA VISIWA

Ripoti kutoka Misri zinaeleza kuwa licha ya malalamiko ya wananchi na upinzani wa mahakama, serikali ya nchi hiyo imepitisha mpango wa kuipatia Saudi Arabia visiwa viwili vya Tiran na Sanafir. Duru za habari za Misri zimetangaza kuwa serikali imeidhinisha mpango huo na tayari imeshaupeleka bungeni.
Kwa mujibu wa duru hizo, Mahakama Kuu ya Misri imepinga mpango huo na inatazamiwa kutoa hukumu yake rasmi juu ya suala hilo katika kipindi cha wiki mbili zijazo.
Baadhi ya shakhsia na wataalamu wa sharia nchini Misri wanaitakidi kuwa uamuzi wa kupitishwa mpango wa kuipatia Saudia visiwa viwili ambavyo Wamisri waliowengi wanaamini ni milki ya nchi yao una uhusiano na kadhia ya kamati za sharia za bunge la Misri.
Ahmad Suleiman, waziri wa zamani wa sharia ameashiria suala hilo na kueleza kwamba lengo la mpango huo ni kukabiliana na mahakimu wanaotoa hukumu kinyume na matakwa ya viongozi wa serikali na badala yake kuzingatia maslahi ya taifa tu. Ameongeza kuwa lengo la serikali ni kuwaondoa mahakimu wanaotoa hukumu zisizoendana na mitazamo ya serikali.

0 comments: