SERIKALI KUANDAA TAMASHA MBALIMBALI JUU YA ELIMU YA KURIDHIA MKATABA WA MATUMIZI YA DAWA ZA KUONGEZA NGUVU MICHEZONI

Na. Lilian Lundo
MAELEZO.
Dar es Salaam
30.12.2016

Serikali kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa  na Michezo pamoja na  Tume ya Taifa ya UNESCO wamekusudia kuandaa tamasha na matembezi mbalimbali ili kutoa elimu kwa jamii kuhusu udhibiti wa matumizi ya dawa na mbinu za kuongeza nguvu michezoni.

Hayo yamebainishwa leo Jijini Dar es Salaam na Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume hiyo,  Dkt. Moshi Kimizi namna ambavyo Serikali imekusudia kuanzisha kampeni hizo ili kuionyesha jamii athari mbalimbali za kisaikolojia na kiafya kwa wachezaji na hasa vijana.

Aliongeza kuwa mwezi Juni mwaka huu, Bunge la Tanzania liliridhia mkataba wa kimataifa wa udhibiti wa matumizi ya dawa na mbinu za kuongeza nguvu katika michezo, hatua iliyolenga kulinda na kuimarisha afya za wanamichezo nchini.

“Kwa kuridhia mkataba huu na kuutekeleza itainufaisha nchi kuweza kuhudhuria mafunzo, mikutano na vikao vya kimataifa na kushiriki katika makongamano yenye maamuzi mbalimbali yanayohusu suala hili” alisema Dkt. Kimizi.

Kwa mujibu wa Kimizi alisema kupitia mkataba huo, wanamichezo, walimu wa michezo na wadau wa michezo wataweza kuelimishwa kuhusu athali za matumizi ya dawa au mbinu za kuongeza nguvu michezoni pamoja na aina ya vyakula au vinywaji ambavyo vina asili ya kuongeza nguvu mwilini.

Kwa upande wake Afisa Michezo, Wizara ya Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo Rashidi Mijuza alisema  kuwa, wanamichezo wengi hujikuta wakiwekewa dawa za kuongeza  nguvu na walimu wao katika chakula au vinywaji bila kujua ili tu waweze kushinda.

Kwa mujibu wa Mijuza alisema Serikali imekusudia kutoa elimu kwa wanamichezo na walimu ili kuondokana na visingizio vya kutojua au udanganyifu ambao umekuwa ukifanyika kwa wanamichezo pindi wanapokuwa katika mashindano mbalimbali.

“Kwa Tanzania kuridhia mkataba huo, nchi itanufaika na mambo mbalimbali katika sekta ya michezo ikiwa ni pamoja na Tanzania kushiriki na kuandaa mashindano mbalimbali ya kimataifa, kupata misaada ya wataalamu, fedha na mafunzo kwa ajili ya utekelezaji wa makubaliano” alisema Mijuza

0 comments: