NKURUNZINZA: HUENDA NIKAGOMBEA TENA URAIS 2020

Rais Pierre Nkurunziza wa Burundi
Rais Pierre Nkurunzinza wa Burundi amesema kuwa, huenda akagombea tena urais kwa kipindi cha nne mfululizo kama wananchi wa Burundi watamtaka kufanya hivyo.
Nkurunziza ambaye uamuzi wake wa kugombea urais kwa kipindi cha tatu mfululizo umeitumbukiza Burundi kwenye mgogoro mkubwa amesema katika mkutano mmoja uliofanyika mjini Rutuna, kusini mashariki mwa Burundi kwamba: "Kwa vile tunaheshimu utawala wa sheria na iwapo wananchi watapitisha kuwa, kugombea tena si kuvunja sheria, na kama wananchi wataomba jambo hilo, hatuwezi kusaliti imani  ya nchi, hatuwezi kusaliti imani ya wananchi.
Aidha amesema, kuna uwezekano katiba ya Burundi ikafanyiwa marekebisho na kuondoa kipengee cha ukomo wa kugombea urais nchini humo na pia kipindi cha miaka mitano uongozini.

Askari wa Burundi wanatuhumiwa kuwanyanyasa vibaya raia

Wakati aliposhiriki kwenye uchaguzi kwa mara ya tatu mfulilizo mwaka 2015, Nkurunziza alidai kuwa kuchaguliwa kwake kwa mara ya kwanza mwaka 2005 kulikuwa kwa kipindi cha mpito baada ya vita vya ndani hivyo alikuwa na haki ya kugombea urais kwa mara ya tatu.
Hata hivyo wapinzani waliilalamikia vikali hatua hiyo na kusema kuwa ni kinyume na makubaliano ya Arusha Tanzania yanayompa haki mtu kuongoza Burundi kwa vipindi viwili.
Maelfu ya wananchi wamekuwa wakimbizi, tangu Rais Nkurunziza alipoamua kugombea urais kwa kipindi cha tatu mfululizo

Tangu wakati huo hadi hivi sasa Burundi imeshuhudia machafuko mengi, huku wataalamu wa Umoja wa Mataifa wakiripoti kutokea kesi chungu za uvunjaji wa haki za binadamu, mateso, udhalilishaji wa kijinsia, kutiwa mbaroni watu kwa umati na kupotezwa bila kujulikana waliko.
Burundi ina historia ndefu ya machafuko baina ya makabila ya Kihutu na Kitutsi yaliyopelekea nchi hiyo ndogo ya katikati mwa Afrika kushuhudi miaka 12 ya mapigano ya ndani yaliyoanza mwaka 1993 na kumalizika 2006 kwa mujibu wa Makubaliano ya Arusha. 

0 comments: