MWAKA MMJA WA GOBIG NA MAFANIKIO MAKUBWA NA HAKUNA NDOTO KUBWA DUNIANI

Picha ya Patrock Tenywa
Na: Meshack Maganga- Mwanzilishi wa GoBigDevelopment Network-Tanzania.
Kwenye Jamii Yetu Imezoeleka kwamba, Mfanikio kwenye maisha yapo ofisni ama kwa kuwa na cheo kikubwa . Katika makala hii fupi, nitaelezea kwa kifupi historia ya GoBigDevelopment Network, kikundi kilichoanza kwenye mtandao wa kijamii na kuwa kundi lenye mvuto na mafanikio makubwa sana kwa wanachama wake.
Nilipoandika makala niliyoipa kichwa cha “Waliofanikiwa Hawaishi Kwenye Sayari Ya Proxima Centauri” Nililezea kwa kifupi jinsi ya kujiamini na kutumia mazingira yetu ya hapa hapa Tanzania ili kufikia malengo na ndoto zetu (Sisi wote tumesikia kauli Mbiu ya Serikali yetu HAPA NI KAZI TU). Nilieleza  jinsi ambavyo watanzania na hasa vijana wanavyoweza kutumia fursa zilizopo kujiondoa kwenye umasikini wa kujitakia na pia kuacha tabia ya kulalamika sana bila kuchukua hatua.
Katika makala ile, nilipata mwitikio mkubwa sana. Kwanza, nilipigiwa simu nyingi na kutumiwa barua pepe nyingi, baadhi ya wasomaji walikuja ‘chemba’ kwa lugha ya mkoloni wanaita in box katika mazingira ya mitandao ya kijamii . Wengi wakipongeza na kuomba kujiunga na GoBig Development Network.
Historia Ya “GoBig Development Network” inaanzia mbali sana miaka saba iliyopita nilipoanza kusoma vitabu vingi na kukutana kitu kinaitwa “The Power of the Master  Mind”, nikaanza kujiunga na makundi mbalimbali kwenye jamii na marafiki zangu wale wenye malengo makubwa na wale ambao wanaona uthamani wa wao kuwepo Dunini, kuwepo Afrika,na zaidi kuwepo ndani ya nchi tukufu,nchi  hii kubwa  ya ajabu na yenye fursa nyingi za kiuchumi  iitwayo Tanzania.
Baada ya kuibuka kwa mitandao mingi ya kijamii ikiwemo “FaceBook, WhatSSAP,Na mingine mingi zikiwemo blogs nikakutana na marafiki wengi sana wanaowaza kama mimi, mwenye kiu ya mafanikio.nikajiunga na makundi hayo. Moja ya makundi ninayokumbuka mpaka sasa ni kundi liitwalo “Wakulima wa kisasa” lilinzishwa Dada Fulani mkulima wa Embe na mihogo. Lilinisaidia sana.
Kimsingi, GoBig Development Network imekuja kuanza rasmi miaka miwili iliyopita,  kwenye ukurasa wangu wa face book, nilikuwa nikiandika ama kuweka picha, kila mwisho wa posti yangu nilikuwa nikiandika Maneno haya ‘GoBig Or Go Home and Watch Tv’. Nikiwa na maana kwamba, binadamu wote tuna uwezo sawa tuliopewa na Mungu na sasa una kuwa na chaguzi mbili, ukiona fursa, ni wajibu wako kuifanyia kazi ili ufanikiwe ama uendelee kukaa nyumbani kwako ukiangalia Tv.
Mwaka 2015, nikafungua grupu la whatssap liitwalo “GoBig Or Go Home” nilianza kwa kuwakaribisha marafiki zangu wachache, tulianza kupeana fursa mbalimbali za hasa kilimo . Tulianza kufundishana fursa za kilimo biashara kama ,kilimo cha matunda, ufugaji wa Ng’ombe, mbuzi, bata mzinga,kuku, ufugaji  wa nyuki,kilimo cha miti nk.  Mwitikio ulikuwa mkubwa sana, kutoka wanachama 8, ambao nilianza nao siku ya jumamosi tarehe 18.12.2015 mpaka kufikia wanachama 67 ilipofika mwezi wa kwanza mwaka huu unaoisha wa 2016.(P.T)

Limekuwa ni Grupu la mfano wa kuigwa, watu wamehamsika sana. Mkazo uliwekwa kwamba kila mtu anae jiunga GoBig, lazima awe na kitu ana fanya huko kwake, yaani awe analima, hata kama ni kwa nusu ekari, awe anafuga hata kama ni kuku watano, ama awe anafuga samaki, nyuki, ana panda  miti nk.
Nilianza kutafuta watu wenye mafanikio makubwa kwenye kilimo, na ufugaji na kuwaomba Muda wao, waje kwenye Grupu la GoBig, ili waweze kutoa hamasa, walikubali bila malipo na kutumia muda wao kuja kutufundisha kilimo hii ikawa mwanzo wa mafanikio makuba sana tuliyoyapata kama kikundi.
Nimekuja kuamini kwamba, hapa duniani HAKUNA NDOTO KUBWA YA KUMSHINDA MWANADAMU ANAEPAMBANA . Nimeamaini tena kwamba maisha yenye mafanikio  ni vitendo na si ndoto pekee, ndoto ni mwanzo tu wa maisha. Maisha ni kuchukua hatua na si kufikiri pekee. Maisha ya kijasiriamali ni kusonga mbele na si kupiga kele za lawama peke yake. Katika yote uliyochagua maishani kuwa mtendaji, usikubali kuyaishi maneno ishi matendo.
Kuanzia mwezi wa pili mwaka 2016, tulianza kufanya ziara mbalimbali za kuwatembelea watu wenye mafanikio kwenye mikoa ya Tanzania bara. Kwanza tulianza na mkoa wa Iringa, tulitembelea vituo vya kilimo kama Baltony, kujifunza kilimo cha umwagiliaji, tuliwatembelea wakulima wa miti, wakulima wa vitunguu na Nyanya na kuweka mkazo kwa kila mwanachama wa GoBig kuanza mchakato wa kufanya uwekezaji kwa kitu anachokipenda. Mwitikio umekuwa mkubwa sana.
Aidha, tulisafiri kwa nyakati tofauti na kwenda mkoa wa Mbeya hasa wilaya ya Rungwe na kukutana na wakulima wakubwa wa Parachichi, Chai, Ndizi, nyanya na ufugaji wa ng’ombe wa maziwa kisasa. Mikoa mingine ambayo tumefika kama kikundi cha wajasiramali ni Mkoa wa pwani, Morogoro nk.
Kwakuwa Asimilia kubwa ya vijana wakitanzania,    wamekuwa wakilalamika sana hasa kwa kukosa mitaji, sisi kwenye kikundi chetu cha GoBig, tumepiga marufuku ulalamishi na akionekana mwanachama anaetoa visingizio vya mitaji tunachofanya ni kumwambia aondoke haraka ili aingie mtaani kulalamika zadi. Jambo la kujuliza ni hili, unalalamika huna mtaji wakati sehemu kubwa ya aridhi yetu Tanzania haijatumika, unaweza kulima matuta matano ya kabichi, ukawa unaingiza hadi laki mbili kila unapovuna. Unaweza kulima mchicha, matuta kumi na baada ya siku kumi na nne ukaanza kupata pesa na ukivumilia ukapata mtaji mkubwa kupitia huo mchicha. Tunakosa mtazamo sahihi wa kipi tunakitaka. Kuna mapori makubwa ndani ya hayo mapori unaweza kufuga nyuki kwa mtaji mdogo sana. Usiseme hakuna pesa, Usisema pesa zimepotea, sema mimi nimepotea, sema sina pesa, pesa zipo nyingi sana, fursa za kumwaga…Unachotakiwa kufanya ni –KUGOBIG.
Miezi mitano baadae yaani Tarehe 17.7.2016, GoBig Development Network Tulipata bahati ya  kumtembelea aliyekuwa waziri mkuu wa awamu iliyopita ,Mh. Pinda, hii ilikuwa ni bahati Ya kipekee sana kwetu. Tulijifunza mambo mambo makubwa sana na hasa ya kubadilisha fikra, ninakumbuka swali moja ambalo Mh. Waziri mkuu mstaafu, alituuliza sisi kama Wana-GoBig, kwamba, “Wanangu hivi inakuwaje mtu ushindwe hata kupanda mashina kumi ya papai?, unashindwaje kuwa na miembe mashina kumi ya miembe kijijini kwenu ? Baada ya ziara hii iliyokuwa na mafanikio makubwa sana kwetu, wengi wetu tulianza kufikiri tofauti.
Kwa kuhitimisha Historia hii fupi ninaweza kusemakwamba kikundi cha  GO BIG DEVELOPMENT NETWORK ni fungamano huru la wajasiriamali wanaoshughulika na shughuli za maendeleo katika nyanja za kilimo,ufugaji wa aina mbalimbali,uwekezaji,na biashara. Na lengo letu kubwa ikiwa ni kuhakikisha tunapiga vita umaskini na umaskini wa kifikra.
HAKUNA NDOTO KUBWA, Chagua kufanikiwa,chagua Ku-Gobig, kijaze kichwa fikra za kufika sehemu ambayo utaona kwamba, maisha yanawezekana. Badilili mtindo wako wa kufikiri na taarifa zinazoingia ndani ya kichwa chako ziwe ni zile zinazokupamoyo wa kufanikiwa. Ikumbukwe kwamba, mafanikio yanatokana na mawazo au wazo la mafanikio. Wazo linatengeneza fursa na kama utabuni wazo jipya kwenye mazingira yako utaibuka kuwa mshindi.
Fursa za mafanikio zina gaharama yake, kuna gharama ya muda, gharama ya pesa, na kama haupo tayari kulipia hizo gharama hizo fursa zitakupita. Uchaguzi unabakia kuwa wako. Binadamu wote wenye mafanikio duniani hawachoki kutafuta..! KARIBUNI SANA-GoBig

0 comments: