KUSHAMIRI VITA YA MANENO BAINA YA DONALD TRUMP NA RAIS OBAMA

Sambamba na kukaribia siku ya kuapishwa rais mpya wa Marekani yaani tarehe 20 ya mwezi ujao wa Januari kumeshadidi vita vya maneno baina ya Donald Trump Rais mteule wa Marekani na Barack Obama rais wa nchi hiyo anayemaliza muda wake wa uongozi.
Rais mteule Donald Trump amemtuhumu Rais wa sasa wa Marekani Barack Obama kwamba, anatoa matamshi ya uchochezi na kukwamisha mwenendo wa ukabidhianaji madaraka. Trump ameandika katika ukurasa wake wa mtadano wa kijamii wa Twitter kwamba, atafanya juhudi zake zote kuhakikisha kwamba, anayapuuza matamshi ya uchochezi ya Obama pamoja na hatua za rais huyo za kukwamisha mambo. Hivi karibuni Rais Obama alitangaza kwamba, ana uhakika kuwa kama Katiba ya Marekani ingemruhusu agombee tena kiti cha uarsi kwa mara ya tatu basi angeibuka na ushindi.
Ikulu ya White House
Zimebakia siku 21 tu kabla ya kumalizika kipindi cha uongozi wa miaka 8 cha Rais Obama ambapo Donald Trump ataapishwa na kuwa Ris wa 55 wa Marekani. Katika kipindi hiki cha mpito ambacho kilianza siku moja baada ya kufanyika uchaguzi wa Marekani Novemba 20 hadi atakapoapishwa rais mpya, Obama amekuwa akifanya juhudi za kuimarisha mambo aliyoyaanzisha.
Hii ni katika hali ambayo, Rais mteule Trump anafanya kila awezalo kuzuia kufikiwa lengo hilo la mtangulizi wake. Kwa mfano katika hali ambayo, Rais Obama alikataa kutia saini ujadidishaji wa vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran, Trump aliibuka na kusema kwa mara nyingine kwamba, makubaliano ya nyuklia na Iran yana madhara.
Rais Barack Obama wa Marekani anayemaliza muda wake
Fauka ya hayo, hatua ya kujizuia serikali ya Obama kupinga kura dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa nayo ilitajwa na Donald Trump kwamba, ni pigo kubwa kwa utawala wa Kizayuni wa Israel. Aidha katika siku zake hizi za mwisho uongozini, Obama ametia saini amri ambayo kwa mujibu wake uchimbaji mafuta katika maeneo ya ncha za dunia utakuwa mgumu mno katika kipindi cha uongozi wa Trump.
Donald Trump na washauri wake wanaituhumu serikali ya Rais Obama kwamba, inakusudia kuchukua maamuzi ambayo yatakwamisha utendaji wa serikali ijayo ya nchi hiyo chini ya uongozi wa Trump. Hii ni katika hali ambayo, serikali ya Obama ina wasiwasi wa kuondolewa urithi wake na mambo iliyoyaanzisha. Newt Gingrich, mmoja wa waungaji mkono wakuu wa Trump alitangaza hivi karibuni kwamba, katika serikali ijayo kwa akali asilimia 70 ya mambo yaliyoachwa na serikali ya Obama yataondolewa na kufutiliwa mbali. Sera za ulipaji kodi, uhajiri, afya, na bima nafuu ya matibabu inayojulikana kama ObamaCare ni miongoni mwa mambo hayo.
Wakati huo huo, utanuaji misuli wa Trump dhidi ya waitifaki wa Washington na vile vile hujuma yake ya maneno dhidi ya Umoja wa Mataifa hususan baada ya kupasishwa azimio katika Baraza la Usalama la umoja huo dhidi ya ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kiyahudi katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu za Palestina ni mambo ambayo kwa hakika yanaonyesha kuweko utendaji tofauti baina ya serikali ijayo ya Trump na ile ya Obama inayomaliza muda wake.
Donald Trump, Rais mteule wa Marekani ambaye ataapishwa Januari 20, 2017
Sambamba na tofauti hii kubwa ya mitazamo baina ya serikali ya sasa na ijayo ya Marekani, hivi sasa walimwengu wanashuhudia kushadidi mashambulio na vita ya maneno kati ya Obama na Trump huku zikiwa zimebakia siku chache tu kabla ya tarehe 20 Januari siku ya ukabidhianaji madaraka nchini humo.
Vita hivyo vya maneno vimeongezeka kiasi kwamba, Julián Castro Waziri wa Nyumba na Ustawi wa Miji wa serikali ya Obama amesema kuwa, Donald Trump ni mtu wa kushukiwa na mfisadi zaidi ambaye amewahi kushinda uchaguzi wa Rais nchini Marekani hadi sasa.
Katika upande wa pili wa sarafu pia, waungaji mkono wa Trump wanaamini kwamba, Obama ameipeleka Marekani upande wa kudhoofika na kulegalega.

0 comments: