HABARI ZA KIMATAIFA, WATU 50 WAFA KWA MAFURIKO KATIKA JAMHURI YA KIDEMOKRASIA YA KONGO

Kwa uchache watu 50 wamepoteza maisha, makumi kadhaa wamejeruhiwa na maelfu ya wengine wamebaki bila makazi kutokana na mafuriko yaliyotokea katika mji wa bandari wa Boma katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Ripoti zinaeleza kwamba, maafa hayo yametokana na mvua kubwa iliyonyesha wiki hii na kusababisha mto Kalamu ufurike na kingo zake kupasuka hali iliyopelekea maji kuzagaa katika vijiji viwili vya kusini magharibi mwa mji wa Boma. Hayo yameelezwa na Theresa-Louise Mambu, Waziri wa Afya wa Jimbo la Kongo ya Kati.
Aidha amewaambia waandishi wa habari kwamba, hasara iliyosababishwa na mafuriko hayo ni kubwa mno na kuongeza kuwa, timu ya uokozi inaendelea na kazi yake huku kukiwa na uwezekano wa kuongezeka idadi ya vifo kutokana na watu wengi kutojulikana waliko.
Mafuriko hutokea mara kwa mara katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo
Baadhi ya wakazi wa vijiji vilivyokumbwa na janga hilo la mafuriko wanasema kuwa, wamebaki bila makazi baada ya nyumba zao kusombwa na maji. Gavana wa Jimbo la Boma amesema kuwa, baadhi ya miili ya waliokufa imesombwa na maji hadi nchi jirani ya Angola.
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imekuwa ikikumbwa na mafuriko mara kwa mara na kusababisha maafa makubwa. Mwaka jana madarzeni ya watu walipoteza maisha yao mjini Kinshasa baada ya mji huo kukumbwa na mafuriko yaliyosababishwa na mvua. 
Wataalamu wa masuala ya hali ya hewa wanasema kuwa, mafuriko na ukame vinatarajiwa kuongezeaka zaidi barani Afrika kutokana na mabadiliko ya tabianchi. 

0 comments: