BURUNDI YATISHIA KUISHTAKI AU NA KUONDOA ASKARI WAKE SOMALIA

Burundi imetishia kuushataki Umoja wa Afrika AU sambamba na kuwaondoa askari wake nchini Somalia wanaohudumu chini ya mwavuli wa Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Afrika Amisom.
Rais Pierre Nkurunziza wa Burundi amesema askari wa nchi hiyo wanaohudumu katika kikosi cha Amisom hawajalipwa mishahara na marupurupu yao kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa na ndiposa serikali yake inataka kuwaondoa nchini Somalia, mbali na kuishtaki AU.
Amesema iwapo kadhia hiyo ya mshahara haitakua imepatiwa ufumbuzi kufikia mwezi ujao, serikali yake haitakuwa na chaguo jingine ghairi ya kuwaondoa askari wa nchi hiyo Somalia.
Burundi ambayo ina askari 5,432 ndani ya Amisom, ni nchi ya pili baada ya Uganda kwa kuwa na idadi kubwa ya askari wa kulinda amani nchini Somalia.
Rais Pierre Nkurunziza wa Burundi
Rais wa Burundi amesema nchi hiyo itaushtaki Umoja wa Afrika kwa kukiuka muafaka uliofikiwa na pande zote kuhusiana na mishahara ya askari wa Amisom.
Amisom ilijikuta katika kipindi kigumu cha kuwalipa mishahara wanajeshi zaidi ya 22 elfu wa nchi za Afrika zilizotuma askari wake Somalia zikiwa ni pamoja na Kenya, Ethiopia na Djibouti, baada ya Umoja wa Ulaya EU kupunguza bajeti yake kwa kikosi hicho cha kulinda amani, kwa asilimia 20 mapema mwaka huu.
Nchi ya Somalia iliyoko katika Pembe ya Afrika imekuwa ikikabiliwa na machafuko kwa miaka kadhaa sasa huku kundi la wanamgambo wa al-Shabaab likitishia pakubwa usalama wa nchi hiyo na hata wa nchi jirani. 

0 comments: