SIRI ZAIDI IPTL HADHARANI

  
siri_39ad9.jpg
Dar es Salaam. Maswali juu ya utaratibu uliotumika kutoa fedha zilizokuwa zimewekwa kwenye Akaunti ya Escrow katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT), kutokana na mvutano baina ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na IPTL yameanza kupata majibu.
Wakati mmiliki kwa Kampuni ya VIP Engineering and Marketing, James Rugemalira ameibuka na kukiri kuwa yeye ni miongoni mwa waliolipwa fedha hizo huku uongozi wa IPTL ukifafanua utata kuhusu mkataba wake na Tanesco na jinsi kampuni hiyo ilivyouzwa jumla kwa Pan African Energy.
Majibu ya Rugemalira
Katika ufafanuzi wake, Rugemalira alisema kati ya fedha zilizokuwa katika Akaunti ya Escrow, yeye akiwa mwanahisa wa IPTL alilipwa Dola za Marekani 75 milioni (Sh120 bilioni), alizoziita 'vijipesa vya ugoro' sawa na asilimia 30.
Alisema baada ya kuuza hisa zake kwa Kampuni ya Pan African Power (PAP) aliruhusu pia asilimia 70 ya hisa za mbia mwenzake, Mechmar kutoka Malaysia ziuzwe pia kwa PAP.

Alisema kwenye akaunti hiyo kulikuwapo na Dola za Marekani 120 milioni, tofauti na kiwango kilichotajwa na Gavana wa BoT, Profesa Benno Ndulu aliyesema fedha hizo zilikuwa Dola 122 milioni.
Rugemalira alisema pia kuwa hatua ya kufikiwa kwa hukumu iliyotolewa na Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam na Jaji John Utamwa Januari 17, mwaka 2014 saa 8: 30 usiku, ilitokana na Waziri wa Nishati kumuomba wamalize kesi zilizokuwa mahakamani.
"Niliiambia Serikali kuwa nyie mmeibiwa na sisi tumeibiwa. Mimi nikawaambia kuwa 'the end justify the means' (jambo la muhimu ni matokeo, si njia ulikopitia), mwisho tulikubaliana kwamba kwa masilahi ya Taifa tumalize kesi hii, na mimi ndiyo nikalipwa hivyo vijipesa vya ugoro," alisema Rugemalira.
Hatua ya kutoa fedha zilizokuwa kwenye Akaunti ya Escrow na kugawiwa kwa VIP Engineering na PAP, imefikiwa huku mkopeshaji wa IPTL, Benki ya Standard Charted ya Hong Kong (SCB-HK), inayodai Dola za Marekani 145 milioni (Sh234.456 bilioni), ikiwa haijalipwa na wala haijajulikana italipwa kwa kutumia kanuni gani.
Itakumbukwa kuwa, baada ya benki za Malaysia zilizokuwa zimeikopesha IPTL kuyumba kiuchumi, deni la benki hizo lilinunuliwa na SCB-HK.
"Tumeridhia kuwa hizo asilimia 70 zichukuliwe na PAP na Standard Charted anadai kwamba yeye ndiye mkopeshaji na dhamana yake ni hiyo mitambo, kitu ambacho siyo kweli. Lakini kama ni kweli aende mahakamani kuthibitisha," alisema Rugemalira.
Hukumu iliyotolewa Februari 12, 2014 na Kituo cha Kimataifa cha Usuluhishi wa Migogoro ya Uwekezaji cha Washington DC, Marekani, ilitaka pande hizo mbili zikae na kukubaliana namna ya kukokotoa gharama ambazo shirika hilo la umeme linapaswa kuilipa benki hiyo.
Chanzo: Mwananchi

0 comments: